Macho ya ulimwengu yameelekea Mashariki ya Kati. Ni vita ya Marekani na Israel, dhidi ya Iran. Matukio makubwa hadi sasa ni kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu (Rahbar) wa Iran, Ali Hosseini Khamenei, mwana wa Sayyid Javad Khamenei, vilevile mashambulizi ya Iran kwenye nchi zenye kambi za kijeshi za Marekani.
Iran, au kwa jina rasmi Jamhuri ya Kiislam ya Iran, mkuu wa nchi huitwa Rahbar (the supreme leader). Rahbar wa Iran huvaa pia kofia ya kuwa kiongozi mkuu wa kidini, cheo hicho huitwa Ayatollah. Kwa Waislam madhehebu ya Shia, Ayatollah ni cheo ambacho hupewa mwanazuoni wa daraja la juu, anayetosha kuwa kiongozi mkuu wa kidini.
Kifo cha Khamenei ni tafsiri kuwa Wairan wameondokewa na Rahbar (Kiongozi Mkuu) wa nchi yao, vilevile Washia wamefiwa na Ayatollah (Kiongozi Mkuu) wa madhehebu yao. Itambulike kuwa Washia ndiyo wanaoongoza Jamhuri ya Kiislam ya Iran.
“Ayatollah Khamenei alikuwa ofisini kwake kila siku. Mara nyingi idara ya ulinzi ilimwomba imhamishe kutoka kwenye ofisi yake kwenda jiji lingine kwa ajili ya usalama wake, alikataa, alisema kama ingewezekana kuwahamisha Wairan wote milioni 90 kwenda jiji lingine, yeye angekuwa wa mwisho kuhamia. Ni wazi hilo lisingewezekana kutekelezwa,” alisema Mwakilishi wa Rahbar wa Iran nchini India, Dk Abdul Majeed Hakeem Elahi, alipozungumza na vyombo vya habari India, baada ya kifo cha Ayatollah Khamenei.
Dk Ilahi aliongeza: “Idara ya ulinzi ilimwomba impe handaki kwa usalama wake, alisema kama ingewezekana kuwaweka kwenye handaki Wairan wote, yeye angekuwa tayari kuingia kwenye handaki, baada ya Wairan milioni 90. Bila shaka, isingewezekana kuwaweka handakini Wairan wote. Hivyo, alibaki ofisini kwake, nyumbani kwake, na asubuhi ndege za kivita za utawala wa Kizayuni na Marekani, zilishambulia ofisi yake, alikuwa na mkewe, mkwewe, na baadhi ya wapwa wake, walifariki dunia wakiwa mashahidi.”
Taarifa ya kifo cha Khamenei inaweza kuwa ya mshangao kwa wengine, lakini si kwa wenye kumbukumbu. Kurudi nyuma kidogo, Juni 2025, yalitokea mapigano baina ya Israel na Marekani dhidi ya Iran. Ni wakati huo, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema walikuwa wanajua mahali Ayatollah Khamenei, alipokuwa amejificha, hivyo akamtaka asitishe mapigano bila masharti.
“Tunajua mahali hasa, huyo anayeitwa ‘kiongozi mkuu’ anapojificha,” Trump aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Truth, Juni 17, 2025. Akaongeza: “Ni shabaha rahisi kumfikia, lakini yupo salama. Hatutamuua, angalau kwa sasa. Lakini hatutaki makombora yalenge raia, au wanajeshi wa Marekani. Uvumilivu wetu unafika mwisho.”
Kutoka kauli ya Trump, kisha Dk Elahi, jambo ambalo linaunga nukta ni kwamba tayari idara ya ulinzi ya Iran ilikuwa inatambua Ayatollah Khamenei hakuwa salama. Na hakuwa akijificha, alishinda na kulala Ikulu, palipo na ofisi, vilevile makazi yake. Na aligoma mpango wowote ambao ungemfanya awe mbali na rada za Marekani na Israel, ambazo tayari zilishammulika.
Yapo maneno ambayo Ayatollah Khamenei aliyazungumza nyakati za mwisho za uhai wake, mbele ya vijana wa Iran, ni baada ya kuwepo vitisho vya kumfikia na kumuua. Alisema: “Maisha yangu yana thamani ndogo. Nina mwili wenye ulemavu. Nina heshima kidogo ambayo ninyi nyote mnanipa. Naviweka vyote hivyo kwenye mstari, tayari kutoa sadaka kila kitu.”
Ndani ya maneno ya Ayatollah Khamenei, ungemwona mtu ambaye alikuwa hahofii kifo. Thamani ya uhai wake, aliiweka daraja sawa na mwananchi mwingine yeyote wa Iran. Zaidi, katika umri wake wa miaka 86, na akiwa amebakiza mwezi mmoja na siku 22, atimize miaka 87, alijiona hakuwa na cha kupoteza, zaidi ya kusimamia misingi na madhumuni ya kuunda na kuendesha dola ya Kiislam kwa utashi na wivu usiopimika.
Kabla ya mwaka 1979, Iran ilikuwa dola ya kifalme kwa miaka 478. Kuanzia kwa Mfalme (Shah) Ismail I, akafuata mwanaye Shah Tahmasp I, kisha Ismail II, Mohammad Khodabanda, Abbas I (Abbas the Great), Safi, Abbas II, Suleiman I, Sultan Hoseyn, ambao wote walikuwa koo ya Safavid. Ukafuata utawala wa koo ya Hotak, halafu zilifuata zama za Safavid na Hotak kugawana miji ya utawala ndani ya Iran. Mwaka 1722, Mahmud Hotak, alimpindua Tahmasp II, aliyekuwa akitawala Qazvin, hivyo koo ya Hotak kuishika Iran yote.
Ilishakuwepo koo ya Afsharid, Zand, Durrani, halafu dola ikashikiliwa na koo ya Qajar kwa Karne moja, miongo mitatu na miaka sita, kabla ya koo ya Pahlavi, iliyopinduliwa mwaka 1979. Aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi hayo, Ruhollah Khomeini, ambaye chini ya uongozi wake, ufalme ulipigwa marufuku, Iran ikawa jamhuri. Khomeini akawa Rahbar (Kiongozi Mkuu) wa kwanza wa Iran. Ayatollah Khamenei ni wa pili.
Jumuiya ya Shia imekuwa kwenye mapambano ya karne zote za tawala za kikoo. Kutoka koo moja hadi nyingine, Washia wa Iran walikuwa wahusika kutoka utawala hadi utawala, mara nyingi kama wapinzani, wakati mwingine wakishirikishwa katika utawala. Mapinduzi yaliyoongozwa na Khomeini mwaka 1979, yalimaanisha ukomo wa manyanyaso na mateso yao ya muda mrefu.
Sasa basi, Shia wanaulinda utawala wao kwa sababu za kihistoria, ustahimilivu wa zama za sasa, na kwa ajili ya ustawi wa madhehebu hayo ulimwenguni, kama yalivyo maono ya Khvajeh Mohammad Kujuji Tabrizi (Shah Ismail I), ambaye ndiye aliyeasisi kampeni ya kuwabadili Waislam madhehebu ya Sunni kuwa Shia.
Tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, kisha mapito magumu ya miaka nane ya vita dhidi ya Iraq (mwaka 1980 – 1988), jambo moja ni uhakika, Iran haijawahi kuivamia nchi nyingine. Isipokuwa, yenyewe huvamiwa na kushambuliwa mara kwa mara na Israel, kwa kusaidiwa na Marekani.
Iran imekuwa ikiwekeza nguvu kubwa katika kujilinda. Imesomesha na inaendelea kusomesha wanasayansi kwa wingi, ambao wamekuwa chachu ya kujitengenezea silaha walizonazo. Zaidi, Iran imekuwa kimbilio la vikundi vinavyopigania ukombozi wa taifa la Palestina, hasa Hamas na Hezbollah.
Tangu kuuawa kwa Ayatollah Khamenei, Iran imekuwa ikifanya mashambilizi makali Israel, vilevile nchi jirani zenye kambi za kijeshi za Marekani; Kuwait, Qatar, UAE, Jordan, Bahrain, Syria na Iraq. Utetezi wa Iran ni kuwa kifungu cha 51 cha Mkataba wa wa Umoja wa Mataifa, kinachoruhusu nchi kujilinda inapovamiwa. Marekani haiipigi Iran kutokea ardhi yake, bali wanatumia ngome zake katika mataifa hayo ambayo yanashambuliwa na Iran.
Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton anasema, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, analazimisha vita dhidi ya Iran ili kubaki madarakani. Wakosoaji wa Trump, wanasema Marekani imeivamia Iran ili kuisahaulisha dunia kuhusu sakata la Mafaili ya Epstein. Trump alikuwa rafiki na mshirika wa mhalifu wa ngono kwa mabinti wadogo, Jeffrey Epstein.