Wakati huu wa mifungo mitakatifu tunapaswa kumrudia Mwenyezi Mungu kwa nguvu zote. Baada ya kujisahau kwa muda mrefu, mwanadamu hana budi kutubu, kuomba msamaha na kufanya matendo ya huruma japo kwa mwezi huu mmoja na siku kadhaa.
Kimsingi muda huu ni mfupi sana ukizingatia kuwa hayo yanatakiwa kufanywa katika maisha yetu yote. Lakini mwezi huu unatukumbushwa namna ya kuishi vema.
Dhambi inayoongoza maishani mwetu ni kunyimana haki. Kila sekunde kuna mtu ananyimwa haki yake kwa kudhulumiwa iwe kwa kuibiwa, kuteswa, kubakwa, kudaiwa rushwa na kadhalika.
Baadhi ya waovu wamefikia kuihalalisha dhambi hii kuwa jambo la sifa kama sunna au faradhi. Hivyo moja ya njia iliyo karibu zaidi katika kumrudia Mungu ni kutendeana haki baina yetu.
Siku iliyotangulia mfungo, wananchi wa maeneo ya Buza walikwenda kwenye vituo vyao vya usafiri wa kuwapeleka kazini, shuleni, hospitali n.k.
Lakini badala ya daladala, walikuta askari wakiwa wakiwa wametanda kituoni hapo. Walifukuzwa na kupewa maelezo kuwa kuanzia siku hiyo kituo chao kimehamishiwa katika kituo kipya cha Mama Kibonge.
Wote walipigwa na butwaa, na walioweza iliwapasa kulipia bajaji au boda mpaka huko kituoni kabla ya kulipia tena safari ya katikati ya mji.
Baadhi ya wasafiri na wasafirishaji waliomba ufafanuzi kwa viongozi wao. Baada ya kuukosa, waliamua kwenda kuupata huko juu kwa wakubwa, lakini vyombo vya dola viliwahi kuwatawanya. Jambo hili lilikuwa kama janga kwao, kwa kuwa baadhi yao hutegemea kufungua biashara zao ndipo wapate pesa ya chakula na nauli ya kurudia nyumbani. Unapomuamuru alipie safari zaidi ya moja unakuwa umemtoa relini.
Kidogo nikudokeze historia ya eneo hili katika miaka ya Tisini. Wakazi wa Buza (wakati huo ikijulikana kama “Soweto”) walilazimika kutembea kilomita saba na zaidi kufuata mabasi kituoni Tandika. Wasafirishaji wakaiona na kuichukua fursa hiyo, wakawasogezea usafiri wa gari ndogo za mizigo (pick-up) zilizojulikana kama “Chai Maharage”. Mwanzoni usafiri huu ulihudumu kutoka Tandika hadi Yombo Abiola.
Sababu ilikuwa ni kutokuingilika kwa Buza. Kulikuwa na mkondo wa maji uliokwenda kuungana na Mto Mzinga, na hapakuwa na daraja. Hatimaye katika awamu ya pili ya uongozi wa nchi, marehemu Ali Hassan Mwinyi alipokuwa madarakani alifungua njia muhimu sana ya Solar Power.
Aliweka makaravati na daraja la muda, gari zilianza kuvuka hadi Buza. Kwa wakati huo ziliishia Kwa Lulenge. Baada ya kuona hivyo, wananchi wakaanza kupeleka maendeleo ya kasi katika eneo hili. Walijenga nyumba bora katika maeneo ambayo sasa ndio Buza Kanisani.
Kama kawaida ya maendeleo, watu wakajiongeza kwa kupeleka huduma na vitega uchumi vidogo vidogo. Wasafirishaji nao wakaona fursa ya kuanzisha safari za Daladala baina ya Tandika na Buza Kanisani.
Hali iliendelea kuboreka katika awamu ya tatu ya mzee Kikwete. Wakati huu ndio ambao daladala zilianza kusafirisha abiria kutoka Buza hadi Kariakoo na Posta.
Wawekezaji waliongeza kasi ya ujenzi wa Hospitali kubwa (kama Aga Khan), Shule za Bweni na vituo vya mafuta. Wengine walijenga maghala maana eneo linapakana na Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.
Katika awamu ya nne ya Mheshimiwa Magufuli, sehemu hii ilizidi kupata neema baada ya kuunganishwa kwa ruti za Mbagala, Kawe, Makumbusho, Ubungo, Mbezi na kadhalika. Huu ndio wakati ambao bandari kavu zilianza kumiminwa, na kuongezeka kwa wawekezaji wa vituo vya kuhudumia magari yatumiayo gesi. Kiramani hasa kwa upande wa usafiri, Buza inaanzia Kwa Mama Kibonge hadi Buza Sigara. Kuzuia magari yaishie Kwa Mama Kibonge ni kukata mawasiliano kutoka hapo, Kwa Lulenge, Hospitali, Kanisani, Tanesco hadi Sigara.
Utaona kuwa kituo hicho kimetengwa ili wakazi wa Buza wakifuate kwa gharama za ziada. Haya hatuwezi kuyaita maendeleo. Itakumbukwa Mheshimiwa Magufuli alipohamisha kituo cha mabasi ya Mkoani kutoka Ubungo kwenda Mbezi, alitengeneza miundombinu rafiki ya kufika hapo. Karibu kila sehemu ya mji ina ruti ya kufika Mbezi bila kuunganisha mabasi. Lakini kinachoendelea Buza kinafanana na kukata ruti. Wanafunzi na wasafiri wengine wanaotoka na kuingia Buza wanalazimishwa kuingia kwenye gharama zisizo za lazima.
Mpango huu unaongeza gharama kwa wananchi ukizingatia huduma muhimu za kijamii zipo Buza Kanisani. Inafika mahala watu wanajiuliza huu ni mpango wa Serikali au wa wafanyabiashara? Kama ni biashara, siku moja watahamishiwa kituo Kwa Mpalange kufuata matakwa ya mfanyabiashara. Si jambo geni kwa vituo kuhamishwa Lakini hayo yanafanyika ili kuboresha huduma za jamii na si kulazimisha mapato.
Ni kama tulivyoona mchakato wa kituo cha mabasi ya mkoani, kila mwananchi alipewa huduma ya kufika Mbezi moja kwa moja.
Hivi sasa watu wanaunganisha ruti za Mloganzira ili wafike hospitali kwa urahisi. Sasa hii ya Buza imekaaje? Ndio maana wasafiri, wasafirishaji na viongozi wao waliandamana kutaka ufafanuzi.