Miaka mitano imepita tangu Othman Masoud Othman alipoingia rasmi kwenye siasa, baada ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Machi Mosi, 2021 kupitia chama chake cha ACT Wazalendo.
Othman, maarufu kama OMO, aliteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki Februari 17, 2021 kiongozi wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar ambaye misimamo yake imeijenga Zanzibar kuwa na mfumo wa siasa uliopo sasa.
Ikumbukwe kwamba huko nyuma, Othman alikuwa ni mtumishi wa umma mwandamizi aliyetumikia katika nafasi mbalimbali ikiwemo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar.
Mwanasiasa huyu ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, hakuwa mwanasiasa kabla ya mwaka 2021. Sasa, ametimiza miaka mitano akiwa mwanasiasa na kiongozi wa juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu kuhusu safari yake hiyo ya miaka mitano katika siasa na ifuatayo ni sehemu ya majibu yake katika maswali aliyoulizwa kuhusu uzoefu huo alioupata katika kipindi hicho.
Nini tathmini yako ya miaka mitano ya safari yako ya siasa?
Jibu: Safari hii imekuwa ya mafunzo, ustahimilivu, na utumishi kwa wanachama wenzangu na wananchi wenzangu pia. Nimepata fursa ya kuuona upande wa pili wa sarafu: kutoka kuwa mwanasheria na mshauri wa kisheria hadi kuwa kiongozi wa kisiasa. Tathmini yangu ni kwamba tumefanikiwa kuendeleza utulivu wa kisiasa Zanzibar, jambo ambalo Maalim Seif aliliwekea msingi kwa gharama ya maisha yake. Nimeimarisha taasisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kuhakikisha sauti ya mabadiliko haipotei ndani ya korido za Serikali, hata kama nilikuwa sehemu ya Serikali. Imekuwa miaka ya kujijenga upya lakini kwa kupita njia tuliyokulia. Njia ya majadiliano, njia ya uzalendo, njia ya kutafuta haki.
Ilikuwaje ukaingia kwenye siasa wakati huo, nini kilikusukuma?
Jibu: Kwanza niweke wazi. Mimi sikuingia kwenye siasa. Mimi niliingizwa kwenye siasa. Sikuingia kwa maana ya kufuata utashi wangu binafsi kwenye siasa kama wanavyoingia wengine kutafuta cheo ama nafasi. Hapana, mimi niliingizwa kwa wito wa kihistoria kutoka kwa Wazanzibari wenzangu. Baada ya kuondoka kwa Maalim Seif, kulikuwa na pengo la uongozi lililohitaji mtu mwenye uelewa wa kina wa masuala ya kisheria na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Na wala si kwamba mimi nilikuwa bora zaidi ya wale wote waliokuwa wamefikiriwa. Lakini wenzangu wakaona mimi nafaa zaidi miongoni mwetu kutumwa na nikawatumikia. Nami nikakubali kuja kumrithi mzee wetu. Marehemu Maalim Seif, na kwa kweli, kilichonipeleka kukubali hasa ni mapenzi yangu kwa Zanzibar na imani kuwa mabadiliko ya kweli yanahitaji watu walio tayari kusimamia misingi ya Katiba, hata kama ni kwa gharama ya maslahi binafsi. Wenzangu walinikubali kwa hilo na ndio maana wakanitanguliza mbele, nami kwa kuwa ni utumishi wa nchi yangu, niliupokea kwa moyo mmoja. Sikuwa na kinyongo. Na kwa kweli, niseme kuwa sijutii uamuzi huo nilioufanya miaka mitano iliyopita.
Kuna tofauti gani kati ya utumishi wa umma na kufanya siasa? Ni wakati upi umeufurahia zaidi?
Jibu: Kwa miaka 25 ya awali ya utumishi wangu Serikalini, nilikuwa mtumishi wa umma kwenye tasnia ya sheria na mambo yanayohusiana nayo. Utumishi wenyewe wa umma ni kufuata sheria, kanuni, na utaratibu, wanavyoita technocracy, kwa Kiingereza. Ukiwa mtumishi wa umma, unasalia kwenye jukumu la mtekelezaji wa uamuzi ulioamuliwa na walio juu yako na au kuwa mshauri kwa eneo lako la utumishi. Lakini huamui muelekeo hasa wa nchi, kama vile sera au dira kuu ya Taifa. Lakini ukiingia kwenye siasa, ninavyoona, hasa kwa nafasi kama ambayo niliwekwa na wenzangu miaka mitano iliyopita, nilipewa jukumu la kubeba maono ya watu. Visheni ya mapambano yetu. Dhamira ya taifa letu. Hapa unaamua mwelekeo na unabeba lawama au sifa za uamuzi huo.
Tofauti nyingine kubwa ninayoiona ni utamaduni na mbinu za kazi. Katika utumishi wa Serikalini, unaongoza wenzako kunyooka katika kufuata kanuni zilizowekwa za kazi. Mkazo ni kutii sheria, kanuni na amri zilizopo.
Katika utumishi wa siasa, tofauti za mtazamo na makundi ndio msingi mkuu. Hivyo, ni lazima uwe na maarifa ya kutambua tofauti za mitizamo na kujua makundi yaliopo na kujenga maarifa ya kuyaendea na kuishi nayo mambo hayo mawili bila mivutano na bila ya wewe kiongozi kuwa sehemu ya tatizo bali kuwa tegemeo la kupata suluhu.
Yapo ambayo nimefurahia kwa dhati katika utumishi serikalini na yapo pia katika utumishi wa siasa. Katika utumishi Serikalini nilipata fursa ya kujenga taasisi muhimu za nchi yetu ikiwemo Wizara ya Katiba na Utawala Bora nikiwa Katibu Mkuu wa mwanzo, Bodi ya Mapato ya Zanzibar nikiwa Mwenyekiti wa mwanzo wa Bodi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nikiwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa mwanzo na Chuo cha Utumishi wa Umma nikiwa pia Mwenyekiti wa mwanzo wa Bodi.
Baada ya kuingia ndani ya siasa, nikiri kwamba yapo mambo mengi ambayo nimefurahia sana katika utumishi wa siasa. Kwanza, utumishi wa siasa umenipa fursa ya kukipigania kile ninachokiamini moja kwa moja. Katika siasa, ninaweza kuwa sauti ya mwananchi wa kawaida ambaye hawezi kufika ofisini kwangu. Naweza kuisimamia maono ya Zanzibar ambayo ndiyo iliyomo nafsini mwangu. Hata kama nilipokuwa kwenye utumishi wa umma niliisimamia na kusababisha kufukuzwa serikalini, lakini kama nisingeliingia kwenye siasa pengine ule ulishakuwa mwisho wa sauti yangu. Ingelibakia kuandika makala hapa na pale, kuwasilisha mada kwenye kongamano hili na lile, lakini kwa kweli ni kama kwamba nilishafikia ukomo wangu kwa njia ile.
Mambo gani mahsusi umeyafanya au kufanikisha tangu umekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar?
Jibu: Kujibu suali hili ni muhimu, kwanza, kuzingatia mipaka na majukumu yangu kama yalivyoainishwa kwenye katiba na pia utamaduni wa kisiasa wa yule ambaye mimi ni msaidizi wake. Kikatiba ni mshauri mkuu wa Rais, ambaye kila uamuzi kuhusu uendeshaji wa nchi napaswa kushirikishwa kushauri. Wakati mwingine, naweza kuagizwa naye kumuwakilisha kwenye shughuli mbalimbali. La kwanza, kwa kusema ukweli lilikuwa halitendeki kikamilifu.
Sikuwa nashauriwa sana kwenye masuala yanayohusu uamuzi ya kisera na uendeshaji wa shughuli za nchi. La pili, ilikuwa mara kwa mara napangiwa kuwa mwakilishi wake kwenye shughuli za kiserikali ndani na nje ya Zanzibar. Lakini hicho ndicho ninachokiita utamaduni wa kisiasa, ambacho lazima kifanyiwe marekebisho ili kuakisi hasa maana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, si kwa sababu alikuwapo Othman tu, lakini kwa sababu ya roho yenyewe ya serikali kama hii. Ambayo ni maridhiano.
Pili, ikiwa utaiangalia miaka yangu minne na kitu ya kuwapo kwenye nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa yale majukumu ambayo yalipangiwa ofisi yangu, tulifanikisha mengi katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kama unavyojua Zanzibar ni nchi ya visiwa, na tumeweka sera madhubuti za kulinda rasilimali zetu. Tulikuwa na mpango wa Zanzibar Green Legacy [Urithi wa Zanzibar ya Kijani], ambao kwangu unanigusa binafsi kando ya kuwa Makamu wa kwanza wa Rais kwa vile mimi ndiye nilikuwa muasisi wa fikra ya kuanzisha Mpango huo. Jingine, ambalo nitaliita ni kujiongeza, maana halimo kwenye majukumu ya kupangiwa, ni suala la maridhiano ya Wazanzibari. Kwa kufahamu kwamba msingi wa serikali ya aina yetu hasa haupo kwenye ushindani wa kisiasa, bali moyo wa maridhiano, nilitumia muda mwingi kuifafanuwa ajenda ya maridhiano na kusimamia kwa dhati ajenda ya umoja, nikihakikisha kuwa SUK haibaki kwenye makaratasi tu, bali inagusa maisha ya watu. Hili huenda halikuwa na mafanikio makubwa sana unapotilia maanani mwenendo wa chaguzi zetu, lakini baadhi ya wakati mafanikio hayahesabiwi kwenye matokeo, bali kwenye jitihada. Nami nadhani kwamba nilijitahidi.
Unajutia mambo gani uliyoyapitia katika kipindi hicho?
Jibu: Sina majuto ya binafsi kama Othman Masoud, lakini nina huzuni ya kimfumo. Nahuzunika kuona kuwa kasi ya mabadiliko ya kidemokrasia bado ni ndogo kuliko matarajio ya wananchi. Kwamba licha ya kuwa na mfumo wa vyama vingi kwa miongo mitatu na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa muongo mmoja na nusu, bado mifumo ya nchi inavuta pumzi ya ubabe, ujambazi na uharamia kwa kisiasa. Mifumo imekataa kustaarabika kwa sababu waliopaswa kushirikiana nao wanafaidika wao binafsi na mifumo hiyo. Kuna wakati unatamani kufanya mambo kwa haraka zaidi, lakini unakumbana na mfumo ambao bado haujajengwa kikamilifu kukumbatia siasa za ushindani wa kistaarabu na unakuwa huna mamlaka ya kubadilisha. Pamoja na kutumia njia mbali mbali za kushawishi na kutumia wenye ushawishi lakini bado hakuna mageuzi ya maana.
Miaka yako mitano ndani ya SUK (Serikali ya Umoja wa Kitaifa) imekuwaje?
Jibu: Nimeshataja kidogo kuhusu SUK, lakini wacha niongezee kidogo. SUK iliasisiwa kwa madhumuni ya kuipa Zanzibar na Wananchi wa Zanzibar fursa ya kutoka katika miaka mingi ya mifarakano na uhasama wa kisiasa ambao hauna msingi halisi bali wa kutengenezwa na kuimarishwa na wanaofaidika binafsi na mifarakano hiyo. Kwa hivyo, SUK ilitakiwa itokane na chaguzi huru, za wazi na zinazoheshimika. Ilitakiwa iwe nyenzo ya kuyajenga maridhiano ya Wazanzibari. Haikutakiwa kuwa kama ndoa ya mkeka, tunavyoiita hapa petu. Ndoa ambayo walioingia wameingia kwa kulazimishwa ama kwa hofu au kwa aibu. Lakini kwa kuwa imekuwa ndoa ya lazima na si kwa maslahi ya taifa, basi ukweli ni kuwa miaka mitano kwenye upande huu ilikuwa ya kuviziana. Kila unapojaribu kujikurubisha kuimarisha umoja, inageuka kuwa kipindi cha vuta-nikuvute. Lakini, alhamdulillah, kuwepo kwake SUK kulikuwa na tija kwa amani ya nchi. Uwepo wangu ndani ya Serikali ulisaidia kuiweka wazi mianya ya ubaguzi, uminywaji wa haki na umetoa nafasi kwa wanachama wa upinzani kujiona ni sehemu ya nchi yao. Haikuwa rahisi, lakini tumeweza kuvuka dhoruba nyingi bila kulivunja jahazi, hata kila ishara ilipokuwa inatupeleka huko. Kama mlivyoona kwenye uchaguzi mkuu na chaguzi za kabla ya hapo. Niseme kwamba tumepevuka pamoja ndani ya SUK na sisi bado tunaamini kuwa ni njia sahihi ikiwa itapitwa kwa dhamira njema na usahihi wake.
Mazungumzo yenu na upande wa pili (CCM) yamefikia wapi? Unaona mwanga mbele?
Jibu: Mazungumzo ni mchakato, sio tukio la siku moja. Tumekuwa na majadiliano ya kidiplomasia kuhusu haja ya kuangalia Mfumo wetu wa kikatiba, Tume ya Uchaguzi, marekebisho ya mfumo na sheria za uchaguzi, na haki za binaadamu na uwajibikaji. Naona mwangaza kidogo, lakini mwanga huo utang’ara zaidi ikiwa upande wa pili utaonyesha utayari wa dhati wa kisiasa kuleta mabadiliko ya kimfumo ndani ya kipindi hiki kabla ya uchaguzi mwingine wowote kufanyika. Niwe mkweli, ilikuwa ngumu sana kuanza na kukubaliana mwelekeo na dira lakini baada ya kuanza tuliona umuhimu wa yale tunayoyajadili kwa mustakabali wa nchi na tumefika mbali. Nina imani tunaweza kuvuka na kuivusha nchi yetu salama ikiwa sote tutasimama katika ahadi yetu ya kuwa sote tunaangalia maslahi mapana ya Zanzibar na Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.
Unaiona wapi Zanzibar ya kesho? Matumaini katika siasa yapo?
Jibu: Zanzibar ya kesho ni ile yenye mamlaka kamili na uchumi imara. Hilo liko wazi kwenye visheni yetu kama chama na yangu binafsi kama kiongozi wa Wazanzibari wanaoamini juu ya Zanzibar mpya, Zanzibar Moja yenye mamlaka kamili. Naiona Zanzibar ambapo kura ya mwananchi inaheshimiwa na ambapo siasa sio uadui bali ni ushindani wa hoja. Matumaini yapo makubwa sana, hasa nikiona vijana wanavyoamka na kutaka mabadiliko. Siasa za chuki zinaelekea ukingoni; siasa za hoja ndizo zinazojenga mustakabali wa Zanzibar ya kesho.
Nini wito wako kwa wanachama wa ACT Wazalendo na Wazanzibar kwa ujumla?
Jibu: Kwa wanachama wenzangu: Msikate tamaa. Mapambano ya haki ni marathon, sio mbio za mita mia. Kwa Wazanzibari wote: Tuendelee kulinda amani yetu, lakini tusichoke kudai haki zetu. Mimi niko hapa kusimamia misingi ile ile ya Maalim Seif: utu, uzalendo, na mamlaka ya Zanzibar. Tushikamane, kwani umoja wetu ndio ngao yetu.