BAADA ya kutambulishwa kuwa kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Shedrack Nsajigwa amesema yuko tayari kuikabili Azam FC, akieleza jinsi alivyoibadili timu hiyo ndani ya uwanja kurejesha ushindi kikosini.
Nsajigwa alitambulishwa kikosini humo akichukua mikoba ya Zedekiah Otieno raia wa Kenya aliyesitishiwa kibarua chake Februari 25, 2026 kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu.
Akizungumza leo Machi 4, 2026, Nsajigwa amesema licha ya kuwa mechi yake ya kwanza kikosini humo, lakini hana ugeni wowote wa Ligi Kuu na amejipanga kuanza vyema kibarua chake baada ya mabadiliko aliyofanya kwa wachezaji.
Amesema anafahamu ugumu wa mechi hiyo kwakuwa Azam ni timu kubwa yenye mastaa wa ndani na nje ya nchi chini ya Kocha Florent Ibenge, lakini hana hofu yoyote na wapo tayari kwa ajili ya kupambana.
“Sijabadilisha kwa ukubwa sana ila yapo mabadiliko fulani kiufundi, tunajua ugumu wa Azam na tunaijua, tuko tayari kuwakabili na kusaka ushindi ili kurejesha nguvu na morali mpya kikosini,” amesema Nsajigwa.
Kwa upande wake straika wa timu hiyo, Samson Mbangula amesema kwa muda mrefu walikuwa wakikosa mabao wanayotengeneza na kuruhusu zaidi wavu wao, lakini wamekuwa na muda mzuri wa kusahihisha.
Amesema matarajio yao kuanzia mchezo ujao kesho dhidi ya Azam wanaenda kufanya vizuri, huku akitoa tahadhari kwa wapinzani akieleza kuwa wachezaji watatimiza vyema wajibu wao kufanya vizuri.
“Tumekuwa na tatizo la kutofunga mabao licha ya nafasi tunazopata, lakini tumekuwa tukiruhusu mabao, kocha amefanyia kazi makosa hayo na kesho tunaenda kufanya vizuri kuanzia kwa Azam,” amesema Mbangula.