Kihongosi aanza ziara Shinyanga, ataja mambo matatu

Shinyanga. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ametaja mambo matatu atakayoyafanya katika ziara yake ya siku nne mkoani Shinyanga iliyoanza leo Jumatano, Machi 4, 2026.

Mambo hayo ni uhai wa chama, kukagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali imepeleka fedha na jambo jingine ni kusikiliza changamoto za wananchi.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akizungunza katika kata ya Isaka jimbo la Msalala, mkoani Shinyanga.



Kihongosi ameanza ziara hiyo baada ya kumaliza ziara kama hiyo hivi karibuni mikoa ya Tabora na Kigoma ambako nako alifanya mikutano, kukagua uhai wa chama na miradi ya maendeleo.

Katika ziara hiyo iliyoanzia Kata ya Isaka Jimbo la Msalala, Kihongosi amesisitiza amani na utulivu kwa wananchi huku akiwataka vijana kutobeba ajenda za watu, wasizozifahamu.

Amesema kila mmoja anapaswa kulinda utulivu uliopo katika mkoa huo na kote nchini.

“Tumekusanyika hapa (Isaka) sababu tuna amani na utulivu, ni wajibu kila Mtanzania kulinda amani tuliyonayo.

“Natoa wito kwa vijana, ninyi ndiyo nguvu kazi, msikubali kutumika vibaya, kubeba ajenda ambazo hamzifahamu,” amesema Kihongosi akishangiliwa kwa nguvu kabla ya kutoa salamu za Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu ambaye kwa mujibu wa Kihongosi mkuu huyo wa nchi atakwenda kufanya ziara mkoani humo.

Leo Kihongosi pia atapokea taarifa ya kazi kwenye ofisi ya CCM kata ya Msalala.

Kisha atafanya ukaguzi wa mradi wa bandari kavu kwenye Jimbo la Msalala na kufanya kikao kwa balozi, kata ya Mwendakulima Jimbo la Kahama Mjini na kukagua mradi wa stendi mpya Kahama Mjini iliyopo kata ya Mhongolo, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara kata ya Nyasubi (Phantom) Kahama Mjini.

Endelea kufuatilia Mwananchi