Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Tarehe 04 Machi, 2026 amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa majengo ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga nchini.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Prof.Mbarawa amesema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kasi inayotakiwa, kwa kuzingatia ubora, ratiba, viwango vya kitaalamu na kimataifa na kuakisi thamani halisi ya fedha.
Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa sana kwenye sekta ya anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege karibu kila mkoa, ununuzi wa ndege na sasa imejipanga kuendelea kuimarisha miundombinu ya mafunzo ya sekta ya anga ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu watakaokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.
“Mradi huu unaotekelezwa kwa shilingi bil. 78 ambao sasa umefikia asilimia 10.3 ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini,tunasisitiza utekelezaji wake kuzingatia ubora, ratiba na viwango vya kimataifa, na kuakisi thamani halisi ya fedha ili chuo hiki kiwe kitovu cha mafunzo ya anga katika ukanda huu,” amesema Waziri Mbarawa.
Mwisho Prof.Mbarawa ametoa rai kwa TCAA kuhakikisha wanawapatia fursa ya mafunzo kwa vitendo vijana wa ndani wanaosoma masomo ya uhandisi na kusisitiza miradi yotr mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa ndani ya nchi itumike kama darasa kwa vijana wetu wanaojifunza ili kuzalisha wataalamu wengi wa ndani kwa maendeleo ya Taifa
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Salim Msangi amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Julai,2023 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa mamlaka hiyo wa kuimarisha uwezo wa ndani katika mafunzo ya anga, sambamba na kuendana na miongozo na matakwa ya mashirika ya kimataifa ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Mha. Stephen Mwakasasa, amesema ujenzi unaendelea vizuri kulingana na michoro na usanifu uliokubaliwa.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo ya mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi wakati wa ziara yake




