Dodoma. Wenyeviti wa vijiji 59 vya Wilaya ya Bahi mwishoni mwa wiki walifanya maandamano hadi ofisi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya, wakitaka kusaidiwa kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Wenyeviti hao wanadai Mkuu wa Wilaya anawafukuza katika nafasi zao bila kuwapa fursa ya kusikilizwa, jambo linalowaathiri katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwatia hofu. Hata hivyo, Thobias Nyingo, amekanusha tuhuma hizo akisema walioondolewa walichukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Amesema wilaya hiyo ina vijiji 59 na vitongoji 502, na waliovuliwa madaraka ni wenyeviti wa vijiji viwili pekee Magaga na Chibelela.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Wilaya ya Bahi, David Makuwa, amesema mkuu wa wilaya hana mamlaka ya kumuondoa Mwenyekiti wa Kijiji moja kwa moja, bali anaweza kuwasilisha tuhuma kwa chama kilichomteua ili zichunguzwe. Iwapo zitathibitika, chama kinaweza kumuondolea dhamana na hivyo kupoteza sifa ya uongozi.
Ameongeza kuwa DC anaweza kumkamata mwenyekiti endapo anahatarisha usalama au kuchochea vurugu, lakini kumuondoa madarakani kunapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu, ikiwamo uamuzi wa wananchi kwa kura zaidi ya nusu.
Akimtolea mfano Mwenyekiti wa Kijiji cha Chibelela, Julius Chilingo, Makuwa alidai aliondolewa katika mkutano wa hadhara bila kuelezwa sababu, na DC akatangaza jina la kiongozi mwingine kuwa kaimu mwenyekiti.
Pia alitaja kikao cha wadau wa maji wa Ruwasa kilichofanyika Januari 28, 2026, ambapo alidai Mwenyekiti wa Kijiji cha Chifutuka alipewa saa sita kurejesha ardhi aliyouza, akitishiwa kuondolewa.
“Hatuna shida na kiongozi wetu kama Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, tatizo ni utaratibu wa kutoa amri ya kumvua madaraka mtu bila kumpa nafasi ya kujieleza,” amesema Makuwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bahi, Stewart Masima, amekiri kuwapokea wenyeviti hao na kusema ataratibu vikao kabla ya kupeleka suala hilo ngazi ya juu. Amesema masuala ya msingi yanapaswa kujadiliwa kwenye vikao rasmi, isipokuwa pale ambapo kuna tishio la usalama.
Kwa upande wake, DC Nyingo amesisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa zilifuata taratibu za kisheria ili kulinda uendeshaji wa serikali za vijiji, huku viongozi wa muda wakisimamia shughuli hadi uchaguzi utakapofanyika.
Waziri wa Tamisemi, Riziki Shemdoe,, amesema hajapokea rasmi malalamiko kutoka Wilaya ya Bahi, hivyo hawezi kutoa maelekezo hadi yatakapomfikia.