Straika wamliza Maxime | Mwanaspoti

WAKATI mashabiki wa Mbeya City wakilia na matokeo yasiyoridhisha, kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime amesema tatizo ni upepo kikosini na ubutu wa straika wake katika kutumia nafasi wanazopata.

Hata hivyo, amewatuliza mashabiki kuwa Mbeya City itarejea vyema kwani ligi haijaisha, huku akionesha kutofurahishwa na baadhi yao wanaoingilia majukumu ya kupanga kikosi uwanjani.

Mbeya City inahaha kwa kukosa matokeo mazuri tangu kuanza msimu huu, ambapo mabosi walifikia uamuzi wa kumtema aliyekuwa Kocha Mkuu, Malale Hamsini na kumvuta kikosini Maxime.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime amesema tatizo ni upepo ambao haujavuma vizuri kwao akibainisha kuwa bado straika wanashindwa kutumia vyema nafasi wanazotenegeneza kupata mabao.

Amesema anafahamu maumivu ya mashabiki kwa matokeo hayo, akifafanua kuwa hafurahishwi na baadhi yao wanaodai kutopanga wachezaji wenye uwezo akieleza kuwa mchezaji yeyote mwenye uwezo atampanga.

“Timu inaenda vizuri, tatizo ni kutumia nafasi kupata mabao, wachezaji wanakosa bahati, haya ni matokeo tu ya mpira, huu ni upepo umetukuta, anapokuja shabiki kusema mchezaji hachezi, mimi ndio nashinda nao mazoezini.

“Bado ligi haijaisha, timu itaimairika na tutakaa sawa, najua wanaumia kwa matokeo ila ndio mpira, tuvumiliane wakati tukiendelea kuisuka vizuri timu na kusahihisha makosa yaliyopo,” alisema Maxime.

Kwa upande wake shabiki wa timu hiyo, Godwin Edgar, alisema hawaridhishwi na matokeo yalivyo licha ya uwapo wa kila kitu, akibainisha kuwa nafasi waliyopo inaongeza presha kubwa kwenye kubaki salama Ligi Kuu.

“Niwaombe wenzangu tusiikatie tamaa, tuendelee kuisapoti timu yetu japokuwa hatuelewi kuna wachezaji wenye uwezo na uzoefu wanakaa benchi, tunaona wengine uwezo wao mdogo lakini ndio wanacheza,” alisema Edgar.

Mbeya City inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 15, imeshinda tatu, sare nne na kupoteza nane.