Majembe saba yampa jeuri kigogo Simba, atuma salamu

LICHA ya Simba kutoka suluhu dhidi ya Yanga katika Dabi ya Karikoo wikiendi iliyopita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Crescentius Magori, amesema usajili uliofanyika dirisha dogo umezaa timu mpya itakayofanya makubwa msimu huu, huku kocha wa zamani wa klabu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akiwataja mastaa watatu wakali.

Simba ilikuwa ugenini wikiendi iliyopita ikivaana na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na matokeo kuwa 0-0 ambayo yamesitisha ubabe wa Yanga iliyoshinda mechi sita mfululizo za Dabi ya Kariakoo katika mashindano tofauti dhidi ya Simba.

Kitendo cha Simba kuonekana kucheza vizuri dhidi ya Yanga na kufanya mashambulizi mengi huku ikitawala mechi kwa asilimia kubwa, kimeibua matumaini si tu kwa mabosi wa klabu hiyo, hata mashabiki wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Magori alisema Simba imeonyesha utofauti mkubwa kwenye mechi hiyo, huku wakianza na wachezaji saba waliosajiliwa dirisha dogo wakiwamo sita wa kigeni ambao wamekwenda kuwanufaisha kwenye mechi hiyo ngumu.

Alisema usajili walioufanya dirisha dogo ni wazi umewalipa kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba walicheza wachezaji wengi wakigeni ambao hii ni dabi yao ya kwanza, lakini wameonyesha hatari kubwa na ubora walionao umetoa ujumbe.


“Uongozi wa Simba nao umefurahishwa na kiwango cha timu ambayo tunayo na itafanya makubwa msimu huu, hilo naliamini kabisa. Kwa sasa ni kama tuna kikosi kipya kwani walicheza wachezaji wapya saba na bado wakafanya vyema.

“Wachezaji wote hawa walisajiliwa dirisha dogo, tunaamini ndani ya muda mfupi tutakuwa na timu bora zaidi, hivyo mashabiki wakae mkao wa kufurahi kwani kuna matokeo mazuri zaidi yanaendelea kuja,” alisema Magori.

Simba dirisha dogo lililofunguliwa Januari 1, 2026 na kufungwa Januari 30, 206, imesajili wachezaji nane. Wawili wazawa Nickson Kibabage na Baraka Mwangosi, huku wa kimataifa ni Clatous Chama, Djibrilla Kassali, Libasse Gueye, Ismaila Toure, Inno Loemba na Anicet Oura. Kati ya hao, walioanza ni Kibabage, Chama, Kassali, Gueye, Toure, Loemba na Oura.

Robertinho alisema Simba sasa ina timu nzuri inayozidi kuimarika, wanacheza kama timu yenye njaa ya ushindi.

“Walikuwa bora kila eneo, kiulinzi, kiungo na hata ushambuliaji. Nimevutiwa na Oura, Loemba na Gueye, ni wachezaji wenye kiwango bora sana tena wakionyesha hilo kwenye dabi,” alisema Robertinho aliyeinoa Simba kuanzia Januari 3, 2023 hadi Novemba 9, 2023.


Kocha huyo ambaye alikuwa wa mwisho kuifunga Yanga kabla ya Simba kuanza kupokea vipigo sita mfululizo akianza pia yeye kupigwa 5-1, alisema ili mchezaji awe bora anatakiwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye mechi kubwa.

“Yanga wamenishangaza na kiwango chao hata kama alikosekana Pacome (Zouzoua) lakini bado hawakuwa bora, walikuwa taratibu sana. Simba ni kama ilikuwa inacheza na Diara (Djigui) pekee kwani ndiye mchezaji wa Yanga aliyefanya vizuri zaidi.

“Tangu nimeijua Yanga huu ndio mchezo ambao walicheza vibaya zaidi na bahati nzuri kwao hawakupoteza, ila bao la Simba ambalo limekataliwa halikuwa ‘offside’, lakini mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu awali aliushika mpira.”