Shinyanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga, imeokoa Sh51.75 milioni, ikiwa ni thamani ya vifaa vya ujenzi wa miradi ya maendeleo, huku ikiendelea na uchunguzi wa mzabuni aliyenunua vifaa bila kuviwasilisha katika mradi.
Hayo yamethibitishwa leo Jumatano, Machi 4, 2026, na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akitoa taarifa ya taasisi hiyo ya robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025.
Kessy amesema Takukuru ilimtaka mzabuni (jina limehifadhiwa) awasilishe vifaa hivyo katika mradi wa nyumba za watumishi wa Shule ya Msingi Magongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
“Katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, Takukuru imefanikiwa kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh51.75 milioni, ambapo mzabuni alinunua bila kuviwasilisha kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi wa Shule ya Msingi Magongwa,” amesema Kessy.
Kessy pia amesema elimu inayotolewa imeongeza uwajibikaji katika idara ya afya ya Halmashauri ya Ushetu na kuongeza mapato kwa asilimia 366, ambapo awali kulikuwa na malalamiko mbalimbali kuhusu upotevu wa mapato.
“Mapato ya idara ya afya yameongezeka kutoka wastani wa Sh3 milioni hadi Sh14 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 366 kwa mwezi, na kuchangia kuboresha huduma za afya.
“Malalamiko 39 yalipokelewa, yanayohusu rushwa ni 22, na 17 hayahusu rushwa. Uchunguzi unaendelea kwa malalamiko yanayohusu rushwa, yale yasiyohusu rushwa walalamikaji wameshauriwa kuyahamishia kwenye idara husika,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, akiwemo Happy Mushi, ameishukuru Takukuru kwa kuokoa kiasi hicho cha pesa, hatua inayothibitisha uwajibikaji wa taasisi.