Bodaboda 3,000 wamepatiwa mafunzo udereva salama Mara

Musoma. Zaidi ya bodaboda 3,000 mkoani Mara wamepatiwa mafunzo ya udereva salama na sheria za usalama barabarani, katika mkakati wa Serikali mkoani humo kupunguza ajali zinazotokana na uendeshaji usiozingatia taratibu.

Awali, bodaboda hao walikuwa wakifanya shughuli zao bila leseni wala mafunzo rasmi ya udereva, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ajali za barabarani.

Hayao yamesemwa mjini Musoma leo Jumatano, Machi 4, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakati alipozindua kambi ya matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kambi inayosimamiwa na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI).

Kanali Mtambi amesema Serikali mkoani humo iliamua  kutafuta suluhisho la kudumu juu ya ajali zilizokuwa zikitokea hasa zilizokuwa zikihusisha bodaboda ambapo uchunguzi wa awali ulibaini wengi hawakuwa na mafunzo rasmi ya udereva.

“Nilitoa maagizo kwenye chuo chetu cha Veta kuanza kutoa mafunzo na kwa vile wengi wamesema hawana uwezo wa kumudu gharama, tuliamua kushusha ada  ya mafunzo kutoka Sh70,000 hadi Sh20,000 ili kuhakikisha kuwa bodaboda wote wanapata mafunzo hayo muhimu,” amesema.

Amesema mafunzo hayo yaliyoanza  kutolewa Desemba mwaka jana tayari yametolewa katika wilaya za Musoma na Bunda na yanatarajiwa kutolewa katika wilaya zote za mkoa huo na hakuna bodaboda atakayeruhusiwa kufanya shughuli hiyo bila kuwa na leseni.

Amesema mabadiliko makubwa yameanza kuonekana hasa kwa maeneo ambayo bodaboda wamekwishapatiwa mafunzo.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya matibabu, Kanali Mtambi amesema Mkoa wa Mara una uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa na bobezi za mifupa, ubongo na mishipa hivyo ujio wa madaktari hao umekuja kujibu changamoto hiyo.

Ameomba kufunguliwa kwa tawi la taasisi hiyo mkoani Mara katika hospitali hiyo ili huduma hiyo iweze kusogezwa karibu zaidi na wananchi hasa wa mikoa ya kanda ya  ziwa, ambao hivi sasa wanalazimika kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Pia, utasaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani, ambazo wananchi wake tayari wameanza kufika mkoani Mara kupata huduma hizo.

“Tangu hospitali hii ianze kutoa huduma takriban miaka mitatu, zaidi ya wagonjwa 200 kutoka nchi jirani wamefika hapa na kupata huduma, tunatarajia wagonjwa wa aina hiyo kuongezeka zaidi pale ujenzi wa hospitali hii utakapokamilika na hii itaboresha mahusiano mazuri ya kidiplomasia kwa majirani zetu kwani wale watakaotibiwa hapa watakuwa mabalozi wema wa nchi yetu huko kwao,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi ya huduma ya madaktari bingwa na bobezi kutoka katika taasisi yake, huduma inayotolewa katika hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke



Awali, akitoa taarifa kuhusu ujio wa madaktari hao, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki  Ulisubya amesema wanatarajiwa kutoa huduma za kibingwa mkoani Mara kwa muda wa siku saba.

Amesema tayari wametoa huduma kwa wagonjwa 231 kwa muda wa siku mbili huku wagonjwa 10 wakifanyiwa upasuaji hali ambayo inaonyesha namna uhitaji wa huduma hizo ulivyo mkubwa katika mkoa huo.

“Kuhusu ombi la kufungua tawi hapa,niseme tayari tumeanza mchakato na ndio maana leo tumekuja hivyo muda si mrefu tutafungua tawi hapa kwani tumeona uhitaji ni mkubwa,” amesema

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa amesema, “ujio wenu hapa pia utaondoa dhana kuwa tiba bora zinapatikana nje ya nchi tu, mimi ni shahidi wa huduma zenu kwani nilipopata ajali mwaka jana nilitibiwa hadi kupona katika hii taasisi na niwapongeze kwa namna mlivyoboresha huduma zenu,” amesema.