Morogoro. Zaidi ya wananchi 1,200 wa vitongoji vya Msufini na Sokoni katika Kijiji cha Kichangani, Kata ya Mhonda wilayani Mvomero, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti Mto Mbulumi uliobadili mkondo na kuingia katika makazi yao, hali iliyosababisha athari kwa zaidi ya kaya 700.
Mafuriko yaliyotokea Februari 26, 2026 yamebomoa nyumba 20, huku nyingine zikiwa katika hatari ya kuanguka. Vyakula, mashamba, mifugo, barabara za mitaa na miundombinu ya maji vimeharibiwa, na kuacha familia nyingi katika hali ngumu.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto, amesema Serikali ina mipango miwili ya kudhibiti mto huo, ikiwemo uchimbaji wa kina na ujenzi wa kingo za mawe ili kuurudisha katika mkondo wake wa asili, endapo bajeti ya takribani Sh7 bilioni itapatikana. Amesema makadirio hayo yanatokana na tathmini iliyowahi kufanywa na aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ilitenga viwanja 120 kwa ajili ya kuwahamisha wananchi wa maeneo hatarishi, lakini hadi mwaka 2024 ni 70 pekee waliohamia kutokana na changamoto za kiuchumi. Kwa sasa, wataalamu wanaendelea kufanya tathmini ya athari, na ripoti inatarajiwa kutolewa Machi 10, 2026 ili kuwezesha hatua za haraka.
Wakazi wamesema tatizo hilo limekuwa la kujirudia kila msimu wa mvua, likiathiri maisha na shughuli zao. Baadhi wamepata majeraha, huku wengine wakiripoti hasara kubwa za mifugo na kilimo. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msufini, Saidi Kizumi, amesema mto huo sasa una njia tano za kumwaga maji na unahitaji kufukuliwa na kujengewa kingo imara ili kuzuia mafuriko, akionya kuwa bila hatua za haraka unaweza kuathiri hata barabara ya Turiani–Morogoro.