Dar es Salaam. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewaondoa wamachinga waliokuwa wakifanyabiashara katika barabara za Uhuru na Msimbazi, eneo la Kariakoo, katika utekelezaji wa tangazo lililotolewa awali kuwataka kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa tangazo lililotolewa na Mkurugenzi wa Jiji, Elihuruma Mabelya, Februari 17, 2026, lililobandikwa katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo.
Tangazo liliwataka wafanyabiashara wanaopanga na kuuza bidhaa katikati ya barabara na njia za watembea kwa miguu kuondoa bidhaa zao mara moja.
Moja ya eneo maarufu kwa uuzwaji wa mitumba katika mtaa wa Msimbazi na Jangwani likiwa limeondolewa meza zilizokuwa zimepangwa mbele ya maduka ya eneo hilo baada ya operesheni kuondoa wamachinga Kariakoo kuanza leo Machi 4, 2026.
Tangazo hilo lilitolewa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuashiria Februari 8, 2026, kwamba ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo utafanyika sambamba na kufunguliwa kwa barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Leo Jumatano, Machi 4, 2026, Mwananchi imeshuhudia barabara za Msimbazi na Uhuru zikiwa wazi kwa watembea kwa miguu, zikiwa na ulinzi wa askari wa jiji na Jeshi la Polisi kuhakikisha utekelezaji wa agizo hilo.
Wafanyabiashara wameonekana kukaa vikundi kuzungumzia hatua hiyo, huku wengine wakijiuliza kuhusu maeneo mapya ya kuendelea na biashara zao.
Akizungumza na Mwananchi, Jumanne Shemdoe, mfanyabiashara wa nguo za mtumba mtaa wa Pemba Kipande, amesema uondoaji umeanza asubuhi baada ya tangazo la wiki mbili.
“Sijafungua mzigo kwa sababu mgambo wanakataza na hadi muda huu sijui kama mtaa niliopo wanakataza au wanaishia Msimbazi pekee, maana kuna muda walisema huku tunaweza kuendelea lakini hatuna uhakika,” amesema Shemdoe.
Amesema tangazo lililotolewa waliliona na kulikuwa na gari linapita kila siku kutangaza, lakini hawakujua utekelezaji ungeanza lini.
Askari wa jiji waliovalia fulana za bluu wakiwa na Jeshi la Polisi katika mtaa wa Msimbazi na Masasi kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anaendelea na shughuli ya kupanga bidhaa barabarani.
Naye, Sabra Kiondo mfanyabiashara wa mtaa wa Narung’ombe na Msimbazi amesema alipigiwa simu na mwenzake kuhusu mgambo kuwaondoa wafanyabiashara eneo hilo, hivyo asiende abaki nyumbani.
“Kuna mwenzangu nafanya naye biashara ya kuuza soksi aliniambia kazi imeanza hakuna haja ya mimi kwenda kwa sababu ya ulinzi uliopo labda nishike mkononi na sio kupanga chini kama awali,”amesema Sabra.
Kwa upande wake, muuza mabegi ya mtumba mtaa wa Msimbazi na Jangwani, Sudi Omary amesema askari walipita na gari na kukusanya meza walizokuwa wakiweka eneo hilo.
Wafanyabiashara wa mitumba katika mtaa wa Msimbazi na Jangwani eneo la Kariakoo wakiwa wamesimama kikundi kujadili kuhusu zoezi linaloendelea la kuwaondoa katika mitaa hiyo.
“Tumefika hapa tumekuta meza zimeondolewa zote pamoja na maturubai ambayo tunafunika kujikinga na mvua na jua, mizigo kuna sehemu huwa tunahifadhi hapa tunafikiria tuingie wapi kuendelea na biashara,”amesema.
Amesema yeye amesajiliwa kwenye mfumo na eneo hilo yupo kwa muda mrefu na hakujua kama atapitiwa kwa sababu siku zote wanaonolewa wale waliopanga barabara ya Msimbazi na wao wanaendelea na shughuli zao, lakini sasa imekuwa tofauti.
Februari 18, 2026, Mwenyekiti wa Wamachinga Kariakoo, Stephen Lusinde alipozungumza na Mwananchi alisema chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni ukiukwaji wa sheria na makubaliano yaliyowekwa na mamlaka husika.
Lusinde ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa alisema wamachinga walishapangiwa maeneo maalumu ya kufanyia biashara na makubaliano hayo yalifikiwa baada ya vikao vingi kati ya uongozi wa wilaya, wakurugenzi na viongozi wa wamachinga.
Alisema kutokana na changamoto za usimamizi, wakati mwingine viongozi wa wamachinga hujikuta wakijisimamia wenyewe kwa kuwazuia wenzao wasivunje sheria, jambo lililowaletea lawama kutoka kwa jamii na mamlaka, wakati hawana mamlaka ya kisheria ya kuchukua hatua kali.
Kwa mujibu wa Lusinde idadi ya wamachinga wanafanyabiashara Kariakoo kwa sasa inakadiriwa kuwa kati ya 13,000 hadi 15,000 wakati waliosajiliwa kwenye mfumo rasmi ni 8,900.