Udhibiti dawa za kulevya Tanga wapunguza waraibu

Tanga. Upatikanaji wa dawa ya kulevya aina ya heroini umeelezwa kuwa mgumu katika Jiji la Tanga, hali inayotajwa kuwa matokeo ya kuimarika kwa udhibiti dhidi ya uingizwaji na usambazaji wa dawa hizo.

Daktari wa afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Wallace Karata, amesema kupungua kwa upatikanaji wa heroini ni ishara ya mafanikio ya juhudi za mamlaka. Hata hivyo, ameonya kuwa uhaba huo umeibua changamoto mpya, ikiwamo matumizi ya dawa bandia zinazochanganywa na valium na kuuzwa kama heroini.

“Matumizi ya heroini yamepungua. Wapo wanaodhani wametumia heroini, lakini vipimo vinaonyesha sivyo. Hii inaonyesha udhibiti umezaa matunda, ingawa kuna hatari ya dawa feki,” amesema Karata.

Kwa mujibu wake, zaidi ya waraibu 1,300 wamesajiliwa tangu kuanzishwa kwa huduma ya methadone mwaka 2020, huku zaidi ya 600 wakipata huduma hiyo kila siku. Amesema huduma hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kupunguza utegemezi wa heroini na kusaidia waraibu kurejea katika maisha ya kawaida.

Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Shaban Miraji, amesema katika Kanda ya Kaskazini kuna vituo vitatu vya tiba saidizi (MAT) katika mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro, huku Manyara ukitarajiwa kupata kituo hicho hivi karibuni. Ameongeza kuwa kituo kingine kinajengwa Muheza kupunguza adha ya waraibu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Wadau wanasema pamoja na mafanikio ya kudhibiti uingizwaji wa heroini, mapambano yanapaswa kuendelea ili kukabili dawa bandia na mbinu mpya za usambazaji. Wanasisitiza ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka, wataalamu wa afya na jamii ili kuimarisha udhibiti na kulinda vijana dhidi ya athari za dawa za kulevya.