KIUNGO mshambuliaji wa Azam, Nassor Saadun amewekwa chini ya uangalizi wa madaktari wa kikosi hicho baada ya kutoonekana uwanjani kutokana na majeraha ya nyama za paja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam, Mbaruku Mlinga, alisema mchezaji huyo amepata majeraha hayo ya kusumbuliwa na nyama za paja ndio maana hajaonekana uwanjani kwa muda sasa, ingawa maendeleo yake ni mazuri na atarejea hivi karibuni.
“Kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa jopo letu la wataalamu ambao wanaendelea kuhakikisha anarejea uwanjani kwa haraka, majeraha yake sio makubwa sana, ingawa tumeona ni vizuri tumpe muda, ili arudi akiwa fiti asilimia 100,” alisema Mlinga.
Majeraha ya nyota huyo yamemfanya kushindwa kuonyesha ubora wake kama alivyofanya msimu uliopita, ambapo kwa sasa msimu huu, amefunga bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Mbeya City, Septemba 24, 2025.
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri msimu uliopita, mashabiki wa Azam walitarajia kumuona, Saadun, akiendeleza tena kile alichokifanya, japo kwa bahati mbaya mambo yamekuwa ni tofauti, kutokana na kiungo huyo kuandamwa na majeraha kwa sasa.
Msimu uliopita wa 2024-2025, kiungo huyo mshambuliaji, alifunga mabao manane katika Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho cha Azam, akishika nafasi ya pili kwa nyota wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga mabao 14.
Mabao manane aliyoyafunga Saadun, yalikuwa ni sawa na yaliyofungwa na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Dodoma Jiji, Paul Peter Kasunda, ambaye kwa sasa anaichezea JKT Tanzania, huku akiwa tayari msimu huu ameifungia mabao matano.