MWENENDO usioridhisha wa Mbeya City kwa sasa katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, zimemweka kwenye wakati mgumu kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime, huku presha ikizidi zaidi baada ya juzi kikosi hicho kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Fountain Gate.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, Mbeya City ilishindwa kutamba nyumbani na kuchapwa bao hilo la dakika ya 77, lililofungwa na Sadick Ramadhan, hivyo kuzidisha presha kwa Maxime kikosini humo.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa kikosi hicho cha Mbeya City, uliliambia Mwanaspoti kwa sasa bado wanaendelea kufanyia tathimini ya kocha huyo, ingawa ni mapema kuzungumzia hatima yake, kwa sababu bado wana matumaini naye makubwa.
“Suala la yeye kumuondoa ni mapema lakini kiukweli ukiangalia mwenendo wetu hadi sasa sio mzuri, nadhani mechi tatu au nne zijazo zinaweza kutupa mwelekeo mpya, ingawa kwa muda huu siwezi kuzungumzia jambo lolote,” kilisema chanzo hicho.
Maxime aliyejiunga na timu hiyo, Desemba 7, 2025, akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Malale Hamsini, aliyeondoka Novemba 30, 2025, ameiongoza Mbeya City katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, huku akishinda moja.
Kocha huyo aliyefundisha Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Ihefu (sasa ni Singida Black Stars) katika mechi aliyoshinda ni ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya TRA United, Februari 7, 2026, huku akitoka sare mbili na kupoteza mbili kati ya tano.
Mbeya City iliyopanda Ligi Kuu ikitokea Ligi Championship msimu wa 2024-2025, ikiungana na Mtibwa Sugar iliyokuwa vinara, kwa msimu huu wa 2025-2026, imeshinda mechi tatu tu, ikitoka sare minne na kupoteza minane, ikiwa nafasi ya 14 na pointi 13.