KOCHA wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, amesema mechi tano zijazo za Ligi Kuu Bara kwa kikosi hicho zitakuwa za uamuzi mgumu wa kuamua hatima yao, japo jambo nzuri kwao kama benchi la ufundi ni kuona ratiba hiyo itaanza kuanzia mwezi ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baresi alisema kutokuwa na mechi yoyote kwa mwezi huu ni jambo nzuri kwa sababu na muda mzuri wa kufanyia kazi makosa mbalimbali yaliyojitokeza, huku wakiboresha maeneo ya kujilinda na ushambuliaji.
“Kadri unavyozidi kupoteza ndivyo ambavyo pia morali ya wachezaji inapungua, tuna muda mzuri wa kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika mechi zetu zilizopita, ili turudi imara na kutoka sehemu tuliyopo,” alisema Baresi.
Katika mechi hizo tano zijazo za KMC, itacheza dhidi ya Mbeya City (Aprili 3, 2026), Singida Black Stars (Aprili 8, 2026), Tanzania Prisons (Aprili 14, 2026), Yanga (Aprili 19, 2026) na Fountain Gate (Aprili 28, 2026).
Baresi aliyejiunga na KMC, Desemba 30, 2025 akichukua nafasi ya Marcio Maximo aliyeondoka Desemba 6, 2025 ameiongoza timu hiyo katika mechi saba za Ligi Kuu msimu huu, ambapo ameshinda moja, sare moja na kuchapwa mara tano.
Kwa msimu wa 2025-2026, Maximo aliiongoza KMC katika mechi tisa za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo alishinda moja, sare moja na kuchapwa saba, huku kikosi hicho kikifunga mabao mawili na kuruhusu 14, akikiacha mkiani na pointi nne.
KMC inayoburuza mkia na pointi nane, imecheza mechi 16 za Ligi Kuu, ambapo imeshinda mbili, ikitoka pia sare mbili na kupoteza 12, huku ikifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25.