Alichokisema Kihongosi ukaguzi ujenzi bandari kavu, stendi Kahama

Shinyanga. Wakati wananchi wa Kahama wakieleza fursa wanazozitarajia miradi ya ujenzi wa bandari kavu na stendi ya mabasi Mbulu itakapokamilika, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetaka kutolewa kwa usawa na haki vibanda vya biashara na wananchi wa Kahama wapewa kipaumbele.

Kauli hiyo ya CCM imetolewa leo Jumatano, Machi 4, 2026 na Katibu Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi alipotembelea ujenzi wa stendi hiyo katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Shinyanga.

Akiwa Kahama katika ziara hiyo, Kihongosi amekagua ujenzi wa bandari kavu na stendi ya mabasi ya Mbulu, amesikiliza kero za wananchi, kuzitafutia ufumbuzi na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya CCM 2025/30.

Katika ukaguzi wa stendi ya mabasi Mbulu uliofikia asilimia 40, Kihongosi ametaka  vibanda vya biashara vitolewe kwa usawa katika stendi hiyo itakapokamilika inayotarajiwa kuwa na wafanyabiashara 700 ikijumuisha vibanda vya maduka 200.

Eneo kunakojengwa bandari kavu,  Isaka Kahama.



Amesema katika utoaji wa vibanda vya biashara, wafanyabiashara wapangwe kwa haki na usawa.

“Mradi ukikamilika tuwapange watu kwa haki, sio viongozi wanahodhi vibanda na wanaostahili hawapati si tabia njema tuwape watu kwa usawa na haki itendeke,” amesema Kihongosi.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi, amesema ameridhishwa na unavyoendelea na kusisitiza ubora wa mradi huo kwa kuyatazama majengo kwa thamani ya pesa inaonekana.

“Ongezeni spidi ya ujenzi, mradi ukamilike kwa wakati,” amesema Kihongosi wakati wa ukaguzi.

Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Kahama, Joseph Mkwizu amesema mradi wa Stendi ya Mabasi Mbulu umefikia asilimia 40 na hadi kukamilika utagharimu Sh27.4 bilioni.

Ujenzi wa stendi ya Mbulu, Kahama ukiendelea.



Amesema mradi huo kwa pamoja unatekelezwa sambamba na miradi ya ujenzi wa kituo cha mabasi Mbulu, ujenzi wa soko la Sango, stendi ndogo Zongomela na soko eneo la viwanda Zongomela.

“Stendi ya Mabasi ya Mbulu itakapo kamilika inatarajiwa kuwa na wafanyabiashara tofauti tofauti 700 ikijumuisha vibanda vya maduka 200 na itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 56,” amesema.

Pia, amesema kutakuwa na eneo la maegesho ya magari madogo ndani ya uzio na nje ya uzio.

Amesema mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa Sh 9.6 bilioni sawa na asilimia 35.2 na kazi imefikia asilimia 40.

Katika ukaguzi wa bandari kavu, Kihongosi amesema kuna maendeleo makubwa Isaka ambayo hakutarajia iwe hivyo, huku akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kiongozi wa mfano katika maendeleo hayo.

“Kwa hali hii, miaka miwili hadi mitano uchumi wa hapa utakuwa zaidi na zaidi,” amesema.

Amewataka wana Isaka kulinda miundombinu hiyo akibainisha kuiharibu maana yake ni kuihujumu na kurudisha nyuma maendeleo yao wenyewe.

“Huu uwekezaji unafaa leo na kwa vizazi vijavyo, ile movement ya mizigo kutokea Dar es Salaam itapunguzwa na itakuwa ikichukuliwa hapa kwenda nchi husika na kupunguza muda.

Eneo kunakojengwa bandari kavu,  Isaka Kahama.



“Vilevile vijana wa Kahama watapata ajira na Serikali itaongeza wigo wa mapato, uwekezaji huu ni wenye tija,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amesema kukamilika kwa bandari hiyo kutasaidia kupunguza bei kwenye bidhaa mbalimbali.

“Italeta fursa, bidhaa kama cement na nyinginezo hatutazinunua kwa bei kubwa kama zamani, bandari hii ni historia, iliyoanza kuzungumzwa zamani hivi sasa inakwenda kukamilika,” amesema Mlolwa.

Wakizungumzia miradi hiyo baadhi ya wananchi wamesema imeleta fursa za ajira na inakwenda kuufungua mji wa Kahama na Mkoa wa Shinyanga kiuchumi zaidi.

Ofisa Usafirishaji wa Mtaa wa Nyakato, Charles Joseph amesema stendi hiyo itaongeza fursa za biashara kwao.

“Katika ujenzi wake, miradi hii imetoa fursa za ajira, lakini itakapokamilika itaendelea kuwa fursa kwetu katika kusafirisha abiria kwenda stendi na hata kwenye bandari kavu,” amesema.

Joshua Boniface amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutawasogezea huduma karibu, hivyo kutatoa fursa kwa mama lishe kuuza chakula, bodaboda kupeleka abiria na hata wajasiriamali wengine kufanya biashara hapo.

Wasome Fidel amesema Stendi ya Mbulu inakwenda kuubadilisha mji huo na kufungua uchumi zaidi wa Kahama kwa kuwa, itakuwa ya kimataifa ikileta mabasi hadi kutoka nchi jirani.