Serikali kuendelea kuwawezesha wanawake kutumia nishati safi

Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayohakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa nishati safi, kuanzia uzalishaji wa majiko banifu hadi usambazaji wa teknolojia za kisasa za kupikia.

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 4, 2026 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima katika kongamano la pili la wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo limefanyika ikiwa ni shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Akihutubia mamia ya wanawake waliojitokeza katika kongamano hilo, Waziri Gwajima amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu ya: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Taifa 2050.’

Amesema kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia katika kufanikisha maendeleo ya Taifa, hasa katika sekta muhimu kama nishati ambayo ni mhimili wa uchumi na maendeleo ya kijamii.

“Takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa, asilimia 81.5 ya kaya nchini bado zinatumia kuni na mkaa kupikia. Matumizi ya kuni yakiwa ni asilimia 55.5 huku mkaa ukiwa asilimia 26.0.

“Ni asilimia ndogo tu ya wananchi wanaotumia gesi, umeme na nishati nyingine safi, hali inayoonesha haja kubwa ya kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati.”

“Kutokana na hilo, Serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeweka ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa, kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034,” amesema waziri huyo.

Hata hivyo, amesema wakati jitihada hizo zikiwa zinachukuliwa, wanawake wameelezwa kuwa waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati zisizo safi kutokana na madhara ya kiafya yatokanayo na moshi pamoja na uharibifu wa mazingira.

Kutokana na hilo, amehimizwa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuongoza mabadiliko ya matumizi ya nishati safi katika familia na jamii zao.

Baadhi ya wanawake Shirika la Umeme (Tanesco) wakiwa katika kongamano la pili  kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia lilofanyika jijini Dar es Salaam.



Hata hivyo, amesema wakati Serikali kupitia Tanesco wameweka mikakati ya kuongeza matumizi hayo hadi kufikia angalau asilimia 20 ifikapo mwaka 2034 kupitia kampeni za uhamasishaji na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo,  maofisa ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya kata hawatakiwi kuachwa nyuma kwa kuwa, ni rahisi kuwafikia wananchi.

“Kuna hii ya majiko ya umeme yanayotumia chini ya uniti moja ya umeme kupika mlo mmoja, jambo linalothibitisha gharama za kupikia kwa umeme zinaweza kuwa nafuu kuliko inavyodhaniwa na wengi.

“Lakini watu hawataweza kulijua hili bila kupelekewa taarifa na moja ya watu wanaoweza kuzifikisha ni maofisa ustawi wa jamii,” amesema Dk Gwajima.

Aidha kwa taasisi za fedha na sekta binafsi amesema ni wadau muhimu katika kufanikisha ajenda hiyo ya nishati safi kwa kuwezesha mikopo nafuu ya ununuzi wa majiko ya umeme.

“Tayari programu mbalimbali ikiwamo mikopo ya majiko kwa wafanyakazi na mpango wa kulipia vifaa kupitia manunuzi ya umeme zimeanza kuleta matokeo chanya.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema nafasi ya sauti na nafasi ya wanawake ndani ya shirika hilo inaheshimika na kuthaminiwa katika ngazi zote za uongozi.

Twange amesema Tanesco inaungana na wanawake duniani kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani kwa kuzingatia ajenda ya haki na usawa kwa wanawake na wasichana na kueleza shirika linaendelea kutekeleza malengo ya maendeleo kwa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika safari ya maendeleo, sambamba na dira ya Taifa ya mwaka 2050.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Lazaro Twange, akizungumza katika kongamano la wanawake wa shirika hilo lilofanyika leo Jumatano, Machi 4, 2026 Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.



Akigusia ajenda ya nishati safi ya kupikia inayosisitizwa na Serikali, amesema wanaunga mkono jitihada hizo kwa kuhamasisha matumizi ya umeme kama nishati safi huku akieleza kuwa, shirika lina mipango ya kugawa majiko ya umeme kwa watumishi wake na kuweka programu maalumu kwa wananchi wanaoingiza umeme majumbani, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama kwa mazingira na afya.

Pia, Twange ametumia nafasi huyo kusisitiza kuwa siku hiyo si ya wanawake pekee wa Tanesco bali ni ya kutambua mchango wao kwa  Taifa, akiahidi kuendelea kusikiliza na kuthamini sauti zao katika kuimarisha utendaji wa shirika.

Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Tanesco, Margareth Mwandu akizungumza kwa niaba ya wanawake wa shirika hilo amesema, katika kongamano hilo zaidi ya watumushi wanawake 1,800 wamehudhuria kutoka mikoa na  vituo mbalimbali vya kufua umeme  pamoja na idara.

Margareth amesema lengo la kongamano hilo ni kuhakikisha shirika linaunga juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupika kwa umeme.

“Sisi wanawake tunajivunia kusukuma agenda ya kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanayolenga kuachana na nishati isiyo salama kwa jamii na Taifa kwa jumla,”amesema.