DK.GWAJIMA ATOA RAI WATUMISHI WANAWAKE TANESCO WAWE VINARA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk.Dorothy Gwajima amewatoa rai kwa wanawake watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wawe vinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Dk.Gwajima ametoa rai hiyo leo Machi 4,2026 wakati wa kongamano la wanawake wa TANESCO, ambapo amesema pia shirika hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo endelevu ya taifa na ustawi wa wanawake, hasa kupitia upatikanaji wa umeme unaorahisisha maisha na kuinua uchumi wa familia.

Akieleza zaidi amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ya kitaifa na haiwezi kufanikiwa bila ushiriki wa sekta zote, akiwemo wanawake wa TANESCO.

“Bila umeme wa uhakika katika kaya nyingi, mwanamke ataendelea kubeba mzigo wa kutumia kuni na mkaa, hali inayohatarisha afya na kupoteza muda wa kushiriki shughuli za maendeleo.

“Takwimu za Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zinaonesha asilimia 81 ya kaya nchini bado zinatumia kuni na mkaa kupikia.Asilimia 55 hutumia kuni na asilimia 26 mkaa,”amesema Dk.Gwajima na kuongeza hali hiyo ni changamoto kubwa inayohitaji mapinduzi ya haraka ya fikra na utekelezaji wa mikakati madhubuti.

Aidha amesema matumizi ya umeme kwa kupikia bado ni madogo, yakifikia takribani asilimia 4.3 tu, huku gesi ikitumiwa na asilimia 9.4 ya kaya. “Nitoe rai kwa TANESCO kushirikiana na wizara yetu na wadau wengine kuhakikisha takwimu hizo zinabadilika kabla ya mwaka 2034.”

Amewakumbusha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, tayari alishazindua mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia wenye lengo la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Pamoja na hayo amesema zipo dhana potofu kwamba kupikia kwa umeme ni gharama kubwa, lakini ukweli teknolojia ya sasa imeleta majiko yanayotumia umeme kidogo na kwa gharama nafuu.

Katika hatua nyingine amesema wizara yake itashirikiana na maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata na vijiji kupeleka elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya umeme kupikia lengo likiwa ni kubadili mitazamo hasi na kuhamasisha jamii kukumbatia mabadiliko hayo.