WAKATI Yanga ikihitaji kuendeleza rekodi nzuri iliyonayo dhidi ya Singida BS leo Alhamisi katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa mkoani Singida, kwa upande wa wapinzani wake, itakuwa na kibarua kizito cha kumaliza uteja wa kupoteza mechi sita mfululizo katika mashindano yote.
Hii itakuwa mechi ya pili kwa timu hizo kukutana mwaka huu, mara ya kwanza ilikuwa Januari 9, 2026 katika Kombe la Mapinduzi huko Zanzibar ambako Singida BS ilipoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Mkongomani, Max Nzengeli.
Licha ya msimu uliopita wa mashindano 2024-2025 Singida BS kuwa tishio kutokana na kikosi chao kusheheni majina makubwa akiwemo Jonathan Sowah ambaye kwa sasa ni mchezaji wa Simba, ilikiona chamoto mbele ya Yanga kwa kupoteza mechi zote tatu.
Ndani ya msimu huo, mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana ilikuwa Oktoba 30, 2024 na Singida BS ilikiona chamoto kwa kuchapwa bao 1-0 kabla ya kupigwa tena jijini Dar es Salaam, Februari 17, 2025 katika mechi ya mzunguko wa pili kwa mabao 2-1. Hizi zote za Ligi Kuu Bara.
Mbali na mechi hizo za ligi, wababe hao walikutana pia katika mechi ya Fainali ya Kombe la FA ambayo ilipigwa Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex na Yanga iliendeleza ubabe wake kwa kutwaa taji kufuatia ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Duke Abuya na Clement Mzize anayeuguza majeraha ya goti kwa sasa.
Mechi nyingine kati ya hizo ambazo Singida BS ilichapwa na Yanga ni nusu fainali ya Kombe la FA, Mei 19, 2024 na wakati huo, Singida BS ilifahamika kama Ihefu, ndani ya dakika 90 mzani ulikuwa sawa kabla ya Stephane Aziz Ki ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad ya Libya kuzamisha jahazi katika dakika ya 116.
Kabla ya mechi hiyo, ukirudi nyuma, Yanga iliinyoa Singida BS kwa mvua ya mabao 5-0 na ndio mechi ya kwanza kati ya sita mfululizo kushinda dhidi ya miamba hiyo ya ukanda wa kati yenye ubingwa wa Kagame 2025 ambao iliutwaa kabla ya kuanza kwa msimu huu wa mashindano 2025-2026.
Kwa kutambua ugumu wa mechi hiyo, Meneja Mkuu wa Singida BS, Othmen Najjar, amekiri wazi kwamba, takwimu haziko upande wao, hata hivyo alisema historia hiyo haiwapi presha, bali inawapa motisha ya kupindua aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakiyapata dhidi ya vigogo hao.
“Sote tunajua ubora wa Yanga, hivyo itakuwa mechi ngumu, naamini matokeo ya mechi iliyopita yameongeza kitu kwa upande wetu, ni wazi kwamba itakuwa mechi tofauti kabisa na iliyopita lakini hii ni nafasi kwa wachezaji kuonyesha yale ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi,” alisema na kuongeza;
“Nina uhakika kwamba tunao ubora wa kushindana na Yanga, ninachotamani zaidi ni kuona watu wa Singida wakiwa nyuma ya timu yao.”
Najjar alisema wataingia uwanjani wakiwa na mtazamo wa kupambana bila kuhofia ukubwa wa wapinzani wao.
“Tunaiheshimu Yanga lakini tutacheza kwa kujiamini na kwa uwezo wetu wote,” alisema.
Alieleza pia ameimarisha safu ya ulinzi na kushambulia kwa pamoja kama timu, akiamini mshikamano utakuwa silaha muhimu kwao. Pia amewataka wachezaji wake kuongeza umakini katika utumiaji wa nafasi.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alieleza kuwa nahodha wake msaidizi, Dickson Job hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na majeraha ambayo alipata katika Dabi ya Kariakoo wikiendi iliyopita Zanzibar.
“Ameumia na atakuwa nje kwa miezi miwili au inaweza kuwa tofauti kidogo, kuhusu Pacome (Zouzoua) kiukweli bado hajakaa sawa, lakini tutaona baada ya mazoezi ya leo (jana) na ni kweli tuna idadi kubwa sana ya majeruhi ila haizuii sisi kujituma,” alisema kocha huyo raia wa Ureno.
Yanga itaingia katika mechi ya leo ikihitaji ushindi ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa inaongoza ikiwa na pointi 29, tofauti ni moja mbele ya JKT Tanzania ambayo ipo nafasi ya pili.
Singida BS mbali na kufuta uteja, itakuwa ikihitaji kusogea nafasi za juu kwani hivi sasa ni ya tisa ikiwa na pointi 19, ushindi utaifanya kusogea hadi nafasi ya sita ambayo ipo Namungo ikiwa na pointi 21.
Licha ya Laurindo Aurelio ‘Depu’ kutofunga katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Simba, bado anasalia kama mshambuliaji hatari zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao matano akicheza mechi tano huku akiwa na asisti moja.
Mshambuliaji huyo ambaye ametua Yanga katika dirisha dogo la usajili Januari 2026, ana wastani wa kufunga katika kila mechi ya ligi, hivyo ukuta wa Singida BS ukiongozwa na nahodha, Kennedy Juma utakuwa na kibarua cha kukabiliana na Muangola huyo ambaye amekuwa akicheza sambamba na Prince Dube.
Kwa Singida Black Stars, moja ya silaha zao muhimu ni Elvis Rupia mwenye mabao mawili na Joseph Guede ambaye alitupia katika mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union. Ni Guede dhidi ya waajiri wake wa zamani.
Ilikuwa kipindi kama hiki cha mvua za masika, 2025 ambapo Singida BS ilikuwa na uzinduzi wa uwanja wake ambao kwa sasa inautumia kwa mechi za nyumbani, Yanga ilialikwa kwa ajili ya mechi ya kirafiki.
Mchezo huo ulianza kama kawaida na Jonathan Ikangalombo wa Yanga akifunga bao la mwanzo katika dakika ya 19 huku Singida ikisawazisha kupitia Marouf Tchakei. Hata hivyo, mvua kubwa ilianza kunyesha mwanzoni mwa kipindi cha pili na ikazidi kupamba moto kiasi kwamba mwamuzi alilazimika kusimamisha mechi dakika ya 57 kwa usalama wa wachezaji na mashabiki, kutokana na hali mbaya ya anga. Timu zote mbili zilikubaliana kutoendelea, sasa ni mwaka mmoja baadae zinakutana tena uwanjani hapo.
Mtihani wa kwanza kwa kocha Shadrack Nsajigwa ndani ya Tanzania Prisons, ni leo dhidi ya Azam iliyotoka kulazimisha sare ugenini dhidi ya Pamba Jiji huku ikienda kumkosa Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Nsajigwa aliyechukua mikoba ya Zedekiah Otieno, hii ni mechi yake ya kwanza kuiongoza Prisons ambayo haina matokeo mazuri msimu huu kiasi cha kuifanya kushika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi 14.
Ushindi wa mechi mbili pekee nyumbani kati ya saba ilizocheza Prisons msimu huu katika ligi, ni mtihani unaomkabili Nsajigwa kuweka hali nzuri mbele ya Azam ambayo haijapoteza mechi yoyote msimu huu kwenye michuano hiyo ikishika nafasi ya tano na pointi 23.
Rekodi zinaonyesha, mechi tano za mwisho baina ya timu hizo, Azam imeshinda nne, huku sare ikiwa moja, hivyo Prisons ina kazi ya kufanya kusaka ushindi wa kwanza baada ya mara ya mwisho kushinda Septemba 30, 2022 kwa bao 1-0 kutoka kwa Jeremiah Juma.
Akizungumzia maandalizi kuelekea mechi hiyo, Nsajigwa alisema licha ya kuwa ni mechi yake ya kwanza kikosini humo, lakini hana ugeni wowote wa Ligi Kuu na amejipanga kuanza vyema kibarua chake baada ya mabadiliko aliyofanya kwa wachezaji.
Alisema anafahamu ugumu wa mechi hiyo kwakuwa Azam ni timu kubwa yenye mastaa wa ndani na nje ya nchi chini ya Kocha Florent Ibenge, lakini hana hofu yoyote na wapo tayari kwa ajili ya kupambana.
“Sijabadilisha kwa ukubwa sana ila yapo mabadiliko fulani kiufundi, tunajua ugumu wa Azam na tunaijua, tuko tayari kuwakabili na kusaka ushindi ili kurejesha nguvu na morali mpya kikosini,” alisema Nsajigwa.
Kwa upande wake straika wa timu hiyo, Samson Mbangula alisema kwa muda mrefu walikuwa wakikosa mabao wanayotengeneza na kuruhusu zaidi wavu wao, lakini wamekuwa na muda mzuri wa kusahihisha.
Alisema matarajio yao kuanzia mchezo ujao kesho dhidi ya Azam wanaenda kufanya vizuri, huku akitoa tahadhari kwa wapinzani akieleza kuwa wachezaji watatimiza vyema wajibu wao kufanya vizuri.
“Tumekuwa na tatizo la kutofunga mabao licha ya nafasi tunazopata, lakini tumekuwa tukiruhusu mabao, kocha amefanyia kazi makosa hayo na kesho tunaenda kufanya vizuri kuanzia kwa Azam,” alisema Mbangula.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge, amekiri mechi dhidi ya Prisons haitokuwa nyepesi akieleza watakuwa makini akibainisha kutokuwapo kwa baadhi ya wachezaji akiwamo Feisal Salum haitakuwa tatizo kwani anacho kikosi bora.
Naye nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda, alisema mechi hiyo itakuwa mgumu kutokana na wapinzani nafasi waliyopo akieleza kuwa hawataki yawakute yaliyowatokea Liverpool mbele ya Wolves walipolala 2-1 juzi Jumanne.
“Bado tuna ubora kwenye Ligi Kuu licha ya ratiba ngumu mfululizo, tunajua ugumu wa mchezo dhidi ya Prisons waliopo chini kwenye msimamo, kila mmoja aliona kilichowakuta Liverpool dhidi ya Wolves,” alisema Mwaikenda.