Global Publishers
March 5, 2026
0 Comments
Manchester United imepoteza kwa mara ya kwanza ikiwa chini ya kocha Michael Carrick baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Newcastle United katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la St James’ Park.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa huku Newcastle wakionekana kupambana kwa nguvu licha ya kubaki na wachezaji 10 kuanzia dakika za mwisho za kipindi cha kwanza.
Dakika ya 45+1, Newcastle walipata pigo baada ya kiungo Jacob Ramsey kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia faulo mbaya, na kulazimika kuendelea na mchezo wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja.
Hata hivyo, kabla ya mapumziko, wenyeji walifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Anthony Gordon dakika ya 45+4. Manchester United walijibu haraka na kusawazisha kupitia kwa Casemiro dakika ya 45+9 na kufanya timu hizo kwenda mapumzikoni zikiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili kilishuhudia Manchester United wakitawala zaidi mchezo wakijaribu kutumia faida ya wachezaji wengi uwanjani, lakini walishindwa kupata bao la pili.
Dakika ya 90, mshambuliaji William Osula aliibuka shujaa kwa Newcastle baada ya kufunga bao la ushindi lililowapa pointi tatu muhimu mbele ya mashabiki wao.
Matokeo hayo yanamaanisha Manchester United wanapata kipigo chao cha kwanza tangu Carrick achukue majukumu ya ukocha, huku Newcastle wakionyesha moyo mkubwa wa kupambana licha ya kucheza muda mrefu wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja.