Katika jitihada za kuchochea ukuaji wa sekta binafsi na kupanua fursa za mikopo kwa wafanyabiashara, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ipo katika hatua za mwisho kuanzisha kampuni maalumu ya dhamana, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika upatikanaji wa mikopo nchini.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema mpango huo unatokana na mafanikio ya dirisha la dhamana lililokuwa likiendeshwa ndani ya benki hiyo kuu, ambalo sasa limekua kwa kiwango cha kuweza kujisimamia kama taasisi huru itakayojulikana kama Credit Guarantee Corporation.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Gavana Tutuba alisema awali BoT ilianzisha mfuko wa dhamana ukiwa na madrisha mawili moja likiwa na lengo la kuwezesha uwiano mzuri katika urari wa malipo na biashara hapa nchini.
“Dirisha la pili ni kwa ajili wajasiriamali wadogo na wa kati ambalo lenyewe ni mahususi kuwezesha wazalishaji kuzalisha kwa kiwango na ubora unaotakiwa kukidhi mahitaji ya soko la ndani ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje (import substitution) ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni,” alisema Tutuba.
Alisema Madirisha yote mawili yapo na mfuko huo na umeendelea kukuzwa na kutoa huduma kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao hawana dhamana za kuweza kukopeshwa na mabenki na kwa wakubwa wanapata dhamana ili kupata mikopo.
Kwa mujibu wa Gavana, madirisha yote mawili yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania Bara na Zanzibar. Wafanyabiashara wadogo ambao hawakuwa na dhamana za kukidhi vigezo vya benki wameweza kupata mikopo kupitia dhamana ya mfuko huo, huku wafanyabiashara wakubwa wakitumia dhamana hiyo kupata mitaji ya kupanua shughuli zao.
Kutokana na ukuaji wa mfuko huo, BoT imeona ni wakati muafaka kuutoa ndani ya benki kuu na kuuanzisha kama taasisi inayojitegemea. “Umeshakuwa mkubwa na una mtaji wa kutosha. Tunatarajia tutaanzisha kampuni hivi karibuni. Ni kama mtoto unamlea anakuwa mkubwa baadaye anatoka nyumbani kwenda kuanzisha mji wake,” alisema Tutuba.
Alieleza kuwa kampuni hiyo itakuwa na idara nne kuu: utawala na usimamizi wa ndani; idara ya dhamana; idara ya historia ya madeni (credit record); na idara ya uandaaji wa maandiko ya miradi.
Upande wa dhamana, Gavana alikiri bado kuna changamoto kubwa katika uchumi wa Tanzania. Wafanyabiashara wengi wanapofika benki kuomba mikopo hukosa dhamana zinazokubalika. Hivyo, kampuni hiyo itakuwa na idara maalumu ya kusimamia dhamana ili kuwasaidia wanaohitaji mikopo lakini hawana mali au nyaraka za kutosha kuwekwa rehani.
Moja ya maboresho makubwa yatakayokuja na taasisi hiyo ni kupanua wigo wa taarifa za wakopaji. Kwa sasa, mfumo wa credit reference unasimamiwa na BoT, lakini taarifa nyingi hutoka zaidi katika mabenki na taasisi chache za kifedha.
“Lazima ifikie hatua tuwe na viashiria ya hatari (risk index) ili mtu anapoenda kukopa warejee wale wanaokopa. Kwa sasa kwenye ‘credit reference’ tunachukua mikopo ya mabenki na sehemu nyingine chache hii tutaipanua ili iweze kuhusika na mikopo yote ndani ya nchi itaonyesha hadi mikopo ya simu na elimu ya juu.
Alisema katika kampuni hiyo moja ya idara itakayoundwa itahusika na masuala ya uandaaji wa maandiko ya miradi na kuwezesha wafanyabiashara na wenye mawazo ya miradi waweze kupata mikopo na hii itakuwa ni mahususi kwa maendeleo ya biashara
“Yote hata ukiangalia maana yake hii iliyokuwa dirisha imekuwa na tunataka ipanuke iweze kufikia watu wote kwa maana ya kuunga mkono uuzaji wa nje na kuwezesha kupunguza utegemezi wa bidhaa nje katika uwanda mpana unaiwezesha kuwa taasisi inayojitegemea”
Alisema kampuni hiyo itakuwa na wanahisa wa nje na tayari wamejadiliana na mabenki baada ya kujifunza kutoka nje na si tu hao kutakuwa na wafanyabiashara na BoT inakuwa inalea na kuipa leseni.
“Imefikia hatua kubwa sana, ilianza kama dirisha sasa inaweza kujiendesha vizuri. Na itaanzishwa mwaka huu, tukianza bajeti mpya mwezi wa Julai iwe imeanza. Tumeshafikia hatua ya juu sana, tayari vikao na wadau wakiwemo maafisa watendaji wakuu wa benki zote ambao walisema ni wazo zuri,”
Alisema uanzishwaji wa kampuni hiyo inaendana na maono ya Rais ya kutaka kuacha tabasamu kwa Watanzania kwani itafikia hatua mtu akihitaji andiko la mradi anaenda kwenye hiyo kampuni akaandikiwa andiko ambalo linakubalika kwenye benki zote.
“Hii itasaidia kupunguza gharama za maandiko ya miradi lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na shughuli ya kufanya ambayo ina mchango katika ukuaji wa uchumi ili kufikia malengo ya dira 2050,” alisema na kusisitiza kuwa taasisi hizo itakuwa haitoi mkopo isipokuwa dhamana.
Swali: Zaidi ya benki 30 zinafanya kazi nchini Tanzania, hata hivyo taasisi mbili zinatawala soko kwa zaidi ya nusu ya mali na faida za sekta hiyo. Unaitathmini vipi hali na ushindani wa sekta ya benki?
Jibu: Hili si jambo la ajabu; matokeo katika sekta ya benki kwa kiasi kikubwa hutegemea mikakati inayotekelezwa ndani ya mazingira ya biashara. Tanzania ipo katika nafasi nzuri, ikiwa na benki 42 zilizopewa leseni zinazofanya kazi kwa sasa nchini. Ingawa ni kweli kwamba benki mbili zinatawala soko, nafasi yao inatokana na mikakati waliyoichagua na kuitekeleza, si kwa sababu ya upendeleo wa kimuundo.
Baadhi ya benki zinazofanya kazi Tanzania zilianzishwa kabla ya vinara wa soko wa sasa, huku nyingine zikiwa zimekuwepo kwa miaka mingi bila kupanuka kwa kiasi kikubwa, hasa kutokana na maamuzi yao ya kimkakati. Mazingira ya uendeshaji ni huru na yako wazi kwa wawekezaji wote wanaotaka kushiriki katika sekta ya benki.
Kama mdhibiti, Benki Kuu ya Tanzania hutoa miongozo mbalimbali ili kuhakikisha benki zinafanya kazi kwa ushindani bila kukumbana na upotoshaji wa soko. Kwa muda sasa tumeanzisha vivutio kupitia mifumo ya udhibiti ili kuhamasisha ubunifu na matumizi ya majukwaa mbalimbali ya utoaji huduma, jambo linalosaidia kukuza sekta kwa ujumla.
Baadhi ya benki bado zinasita kupanua huduma katika maeneo ya vijijini kutokana na hofu ya hatari na gharama. Benki huingia sokoni zikiwa na malengo tofauti: nyingine hulenga wateja wadogo huku nyingine zikijikita kwa wateja wakubwa na kampuni. Hivyo, si rahisi kwa mdhibiti kuziamuru benki zote kufuata mtindo mmoja wa biashara.
Kwa kutambua hatari zilizopo katika sekta, Benki Kuu hufanya usimamizi wa karibu na mawasiliano endelevu na benki, ikitoa mwongozo wa kulinda uthabiti wa mfumo huku ikizipa taasisi uhuru wa kukua kulingana na mikakati yao.
Swali: Kutokana na Serikali kuwa na umiliki wa hisa katika benki hizo mbili zinazoongoza na mara nyingi kuzitumia kufadhili miradi ya umma, je utegemezi huo mkubwa unaweza kuibua hatari za ukwasi katika mfumo wa benki?
Hali kama hiyo haiwezi kutokea. Tunafanya ufuatiliaji wa karibu na tumeweka hatua za kupunguza hatari ili kuhakikisha benki hazishindwi kutimiza wajibu wake. Kupitia uchambuzi wetu, tunahakikisha benki zote zinakuwa na ukwasi wa kutosha na zinazingatia kiwango cha chini cha akiba kinachotakiwa kisheria.
Benki hizo mbili zilianzishwa awali kwa lengo la kuhudumia maeneo ya vijijini, jambo lililowawezesha kujenga mtandao mpana wa matawi na huduma unaowapa faida ya ushindani hadi leo. Hali hii ni tofauti na benki mpya ambazo zimejikita zaidi mijini na kulenga sehemu maalumu za soko.
Kwa kutambua muktadha huu, Benki Kuu imeweka mifumo madhubuti ya usimamizi, ikiwemo ufuatiliaji wa kila siku, mapitio endelevu na hatua za ufuatiliaji katika sekta nzima. Uwezekano wa utovu wa nidhamu ni mdogo, kwa kuwa sekta ya benki inasimamiwa kwa karibu na kudhibitiwa kwa umakini.
Swali: Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya benki imeonyesha ukuaji mkubwa wa faida, ikiweka rekodi mpya mara kwa mara. Hata hivyo, sehemu kubwa ya faida hizo inatokana na mapato yasiyotokana na riba. Kuna maoni yanayoibuka miongoni mwa wananchi kwamba huu ni wakati muafaka wa kuondoa baadhi ya tozo za benki na kupunguza viwango vya riba. Je, Benki Kuu inauchukuliaje mjadala huu?
Wakati uchumi unafanya vizuri, biashara katika sekta mbalimbali hunufaika. Faida ya sekta ya benki kwa kiasi kikubwa ni kielelezo cha uimara wa uchumi, kwani inaonyesha watu wanapata mikopo, wanawekeza kwa tija, na wanarejesha mikopo pamoja na riba.
Tanzania ilipitisha mfumo wa uchumi wa soko huria mwaka 1992. Chini ya mfumo huu, si jukumu la mdhibiti kuweka ukomo wa viwango vya riba vinavyotozwa na benki. Badala yake, jukumu letu ni kuweka mazingira yanayochochea shughuli za kiuchumi huku tukihakikisha viwango vya riba vinabaki kuwa vya busara na vya ushindani.
Ili kuongeza uwazi, Benki Kuu imeanzisha mifumo ya ndani kama zana ya kulinganisha bei, kinachowezesha wateja na wadhibiti kulinganisha ada na tozo kati ya benki mbalimbali. Hatimaye, uamuzi wa mteja kuchagua benki unategemea unachokitaka.
Sisi tunaendelea kuunga mkono sekta nzima ya benki kwa kuhakikisha kuna uwanja sawa wa ushindani na fursa zinazolingana kwa taasisi zote kufanya kazi kwa ushindani ndani ya mazingira hayo hayo.
Viwango vya riba ya mikopo nchini Tanzania, ambavyo kwa sasa wastani wake ni takribani asilimia 15, vikilinganishwa na nchi nyingine, vinaonekana kuwa vya wastani. Katika baadhi ya nchi za Afrika, viwango vya riba vinaweza kufikia hadi asilimia 27.