Tanzania inavyoweza kukabili ongezeko bei ya mafuta duniani

Februari 28, 2026, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi yao kwa Iran, yaliyosababisha vifo vya kiongozi mkuu wa taifa hilo, Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Iran.

Baada ya mashambulizi hayo Iran ilianza kujibu ikilenga kambi za kijeshi za Marekani na Israel lakini pia maeneo ambayo mataifa hayo ya maslahi, Hivi sasa vita hivyo vimesambaa mashariki ya kati na kutatiza mnyororo wa usambazaji wa mafuta na gesi baada ya ghuba ya Hormuz inayopitisha asilimia 20 ya mafuta yote duniani kutopitika hivi sasa.

Kutokana na hali inayoendelea dunia inazidi kushuhudia athari za kiuchumi, Tanzania kama nchi inayotegemea nishati ya mafuta na bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi nayo inatarajiwa kukumbwa na changamoto lakini wachambuzi wanaeleza ni kwa namna gani tunaweza kuepuka changamoto hizo sasa na siku zijazo hususani katika bidhaa ya mafuta.

Wengi wanaamini kuwa pengine Tanzania isingekuwa kati ya nchi zenye hofu juu ya namna zinavyoweza kuathiriwa na mapigano haya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, kwani inayo hifadhi ya gesi asilia ambayo ingeweza kutosha kuendesha shughuli zake za kila siku.

Tanzania inakadiriwa kuwa na akiba ya gesi asilia inayofikia takriban futi za ujazo trilioni 57.4 kufikia Januari 2024. Hata hivyo hutegemea zaidi mafuta yanunuliwa nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha mashine na mitambo katika uzalishaji mali.

Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2025/26 inaonyesha hadi Aprili mwaja jana mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini uliongezeka kutoka kilomita 102.54 mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 Aprili 2025.

Kukua kwa mtandao huo kumewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57. Pia, zaidi ya vyombo vya moto 15,000 vinatumia gesi asilia, hivyo kupunguza mahitaji ya petroli na dizeli katika uendeshaji wa vyombo vya moto nchini.

Hilo limeenda sambamba na kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia nchini kutoka futi za ujazo bilioni 59.83 mwaka 2020/21 hadi futi za ujazo bilioni 82.91 Aprili 2025.

Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa Uchumi, Balozi Morwa anasema mapigano hiyo yataathiri Tanzania kiuchumi ikiwa yataendelea kwani bado mafuta yanatumika maeneo mengi.

Wakati Tanzania ikihitaji mafuta hayo, nchi zinazozalisha zitapunguza uzalishaji kwani zitakosa namna ya kufikisha bidhaa hiyo sokoni wakati wao wakiyahitaji kuendeshea mitambo yao.

“Sasa sisi tunaotegemea mafuta hayo tutaathiriwa kutokana na kupanda kwa bei zake ambazo zitachochea kupanda kwa bei za bidhaa na huduma,” anasema.

Akizungumzia namna gani gesi ingeweza kuwa msaada katika kipindi hiki Morwa anasema kama jitihada zilizokuwa zimewekwa awali zingeenda sambamba na kubadili mifumo ya uendeshaji ikiwemo mifumo ya petroli katika magari na viwanda kuwa gesi ingekuwa na manufaa.

“Lakini sasa ukisema tuwekeze wakati iliyowekezwa awali haijaleta tofauti ni kama matumizi mabaya ya fedha za serikali,” anasema.

Amesema awali wakati gesi hiyo inagundulika na kuanza kuchimbwa, zilitolewa ahadi nyingi kama kumaliza matatizo mbalimbali ikiwemo kuweka historia ya kukatika kwa umeme jambo ambalo liliendelea kushuhudiwa mara zote.

“Tunashindwa kuelewa labda upatikanaji wa gesi na uwekezaji unaofanywa na serikali haujaweza kutatua changamoto zilizokuwepo. Kwanini hakuna tofauti, tuliambiwa kukatika kwa umeme kutakuwa historia lakini ulikuwa unakatika,” anasema.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora anasema mapigano haya yanakumbusha kuwa uchumi wa dunia ni kutegemeana kati ya nchi moja na nyingine na nchi moja anapoguswa kuna zinazo athirika moja kwa moja.

Anasema kinachoendelea katika nchi za Magharibi matokeo yake yataonyesha namna gani nchi za Afrika zimeshindwa kuvumbua teknolojia zao ili kutatua changamoto walizonazo.

“Bado tunategemea kutoka nje, kwenye kesi hii ni fundisho, visima vya wenzetu tunaowategemea kupata mafuta wana mapigano, hii inaweza kufanya hata viwanda vyetu kukwama kama hatutapata visima vya mafuta kwa sababu usambazaji unahitaji mafuta na hili pengo litatufikia,”

Anasema kuna wakati baadhi ya watu walidai kuwa kwenye gesi kuna mafuta hivyo huenda baadaye Tanzania ikawa na uwezekano wa kuwapo kwa mafuta hayo lakini bado inaweka ugumu kuchimba kwa sababu ya kukosekana kwa teknolojia.

“Tuwekeze zaidi katika teknolojia ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji uwe wa mafuta au gesi. Lakini hiki kimetokea wakati bado hatujajiandaa vya kutosha na hatuwezi kusema harakaharaka tupeleke gesi mikoani lakini ingeweza kuwa na msaada mkubwa kipindi hiki tusingekuwa kati ya wanaolia na mabadiliko ya bei,” anasema.

Anasema wakati nchi hizo zikipambana kujiokoa ni vyema Tanzania nayo ipambane kujikomboa kuhakikisha inajitoa katika utegemezi wa mafuta kutoka nje ikiwemo kuongeza utafiti wa mafuta yake na uchakataji wa gesi asilia iliyonayo.

Anasema hali hiyo pia itumike kama chachu kuibua teknolojia zinazoweza kusaidia kuzalisha nishati ya uhakika ikiwemo kutoka katika gesi, jua, upepo ili kuhakikisha nchi inaweza kujitegemea.

Mchambuzi wa Uchumi, Oscar Mkude anasema gesi asilia ni mbadala wa karibu sana wa mafuta na kwakuwa inatoka ndani ya nchi gharama za usafiri pamoja na ushuru wa forodha ambazo huongeza bei kwa mtumiaji wa mwisho zisingekuwepo.
 Amesema upangaji wa bei ya gesi huhusisha sekta mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambao huhusika kukusanya, kununua na kusimamia gesi kutoka kwa wazalishaji mbalimbali.

 “Kwenye gesi hufanyika Tanzania sasa inapotokea hali ya dharura ni rahisi kwa mamlaka za serikali kuangalia ni namna gani wanaweza kuweka unafuu kwa watumiaji. Serikali na mamlaka zake zina uwezo mkubwa wa kudhibiti bei za gesi ukilinganisha na mafuta, hasa katika kipindi cha dharura kama hiki,” anasema.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kujilinda inapotokea misukosuko duniani.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo Machi 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta huku akisisitiza kwamba hifadhi hiyo itaisaidia nchi inapotokea misukosuko duniani kama ilivyo wakati huu.

“Wizara ya Nishati, iimarishe akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kujilinda dhidi ya misukosuko ya kimataifa ikiwemo mabadiliko ya bei. Kama tunavyoona misukosuko iliyotokea hapa karibuni, wiki iliyopita na tunayoendelea nayo, tayari imeshapandisha bei ya mafuta kwa asilimia 13 mpaka jana, sasa hatujui leo na siku zinazofuata,” amesema Rais Samia.