Mbeya. Alfajiri ya Nonde jijini Mbeya, huanza kwa sauti ya mafuta yanayochemka kwenye karai jeusi. Mwanga hafifu wa jiko la mkaa humulika uso wa Rehema Mwanjonde (30) huku mikono yake ikichanganya unga kwa ustadi.
Kabla ya jogoo kuwika mara ya pili, maandazi ya kwanza huwa tayari yameiva, ya moto, yenye harufu inayochochea hamu ya mteja kuyanunua hata kabla hajayaona.
Wakati watoto wake wawili wakijiandaa kwenda shule, Rehema tayari huwa ameshaanza safari ya siku. Hubeba beseni lake kichwani au mikononi, akipita mitaa mbalimbali ya Kata ya Nonde kwa hatua za kujiamini. Kwenye kila kona, sauti yake husikika kwa kibwagizo kilichozoeleka: “Mpende mwanao, mpe ya leo leo, ya moto!”
Ni kauli rahisi, lakini imekuwa alama yake ya biashara na ishara ya mapenzi yake kwa watoto.
Kauli yake ya hamasa ni wazi: “Ujane usiwe sababu ya kutelekeza watoto na kukimbilia ndoa mpya. Mwanamke ni kupambana; kazi ni kazi.”
Miaka minne iliyopita Rehema anasema, maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kufiwa na mumewe.
Ameyasema haya alipofuatwa na Mwananchi nyumbani kujua simulizi ya maisha yake, hususan biashara anayoifanya ya kuuza maandazi ambayo imekuwa simulizi kutokana na staili yake ya kuyanandi mitaani.
Rehema anasema mumewe alimuachia watoto wawili waliokuwa bado wadogo, na mzigo wa majukumu yote ukamwangukia mabegani mwake.
Anasema siku za mwanzo zilikuwa ngumu kupita maelezo, majonzi, upweke na hofu ya kesho yake vilikuwa kama wingu zito kwake.
“Nilijiona sina mwelekeo. Nilikuwa namtegemea sana mume wangu. Alipokufa mipango yote ya maisha iligoma. Watoto walipouliza jambo fulani na kumtaja baba yao, moyo wangu ulikatika, nilikuwa nalia sana kama kichaa,” anasimulia kwa sauti ya utulivu iliyojaa kumbukumbu.
Katika kipindi hicho, anasema aliingia kwenye matumizi ya pombe kama njia ya kusahau machungu.
Hata hivyo, familia yake iliona mabadiliko hayo na kuamua kumsaidia. Walimkalisha, wakamshauri na hatimaye wakampa mtaji wa Sh20, 000 ili aanze biashara ya kukaanga maandazi.
Mtaji huo mdogo ulihutumika kununuia unga kilo tano, mafuta, kuni na mahitaji mengine ya awali. Hakukuwa na uhakika wa mafanikio, lakini kulikuwa na matumaini.
“Siku za kwanza nilipata faida ya Sh4,000 hadi 5,000. Haikuwa kubwa, lakini ilinipa moyo. Nilijua nikiendelea, nitafika mbali,” anasema.
Rehema ambaye hakuweza kuhitimu elimu ya sekondari; alimaliza kidato cha pili mwaka 2000 baada ya kupata ujauzito akiwa katika umri mdogo.
Anasema wazazi wake hawakukata tamaa, lakini mazingira ya maisha yakamzuia kuendelea. Leo anatamani angepata nafasi ya kuendelea na masomo, lakini badala ya kulalamika, ameigeuza hali hiyo kuwa chachu ya kujifunza kupitia uzoefu wa maisha na biashara.
Kadri siku zilivyosonga, anasema aligundua kuwa biashara si kukaanga maandazi pekee, bali ni ubunifu, nidhamu na uhusiano mwema na wateja.
Aliamua kujiunga na michezo ya upatu mtaani kwao, huku akiweka akiba kwenye kibubu. Taratibu, mtaji wake ukakua. Kutoka Sh20,000 hadi kufikia Sh200,000 alizonazo sasa.
Kwa sasa, ana uwezo wa kutumia hadi kilo 25 za unga kwa siku. Anapopika kiasi hicho, hushirikiana na vijana wa mtaani wanaotembeza maandazi katika maeneo mbalimbali. Ujira wao hutegemea mauzo ya siku husika.
“Biashara ikiwa nzuri, nao hupata zaidi. Hivyo tunakua pamoja,” anasema.
Kwa siku yenye mauzo mazuri, Rehema anasema anaweza kupata faida ya Sh40, 000 hadi Sh50,000. Siku zisizo na bahati, hupata kati ya Sh15, 000 na Sh20,000. Mapato hayo huyagawanya kwa umakini kwa ajili ya kununua chakula na mahitaji ya nyumbani, ada na mahitaji ya shule, akiba na uwekezaji mdogo wa ufugaji wa nguruwe na kuku aliouanzisha.
Anasema mafanikio hayo hayajaja kwa urahisi. Kuna nyakati bei ya unga hupanda, wateja hupungua au mvua kunyesha na kuathiri mauzo. Lakini hajawahi kufikiria kuacha.
“Nimejifunza kuwa changamoto ni sehemu ya safari. Ukikata tamaa, umeshindwa. Ukisimama tena, tayari umeshinda,” anasema kwa msisitizo.
Kuhusu ndoto zake, Rehema anatamani kuwa mfanyabiashara mkubwa wa maandazi ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya.
Anapenda kufungua duka maalumu litakalotambulika kwa ubora na usafi, huku akiendelea kutoa ajira kwa vijana zaidi. Anaamini kuwa biashara ndogo inaweza kukua na kuwa kubwa iwapo itasimamiwa kwa nidhamu na uaminifu.
Changamoto kubwa anayoiona sasa, anasema ni ukosefu wa mtaji wa kutosha kupanua biashara. Anaomba halmashauri kuwatambua wanawake wajasiriamali ili wanufaike na mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Wanawake wengi tuna bidii. Tukipata mitaji na mafunzo, tutafika mbali zaidi,” anasema.
Kuhusu suala la kuolewa tena, Rehema yuko wazi. Anasema kwa sasa si kipaumbele chake. Anaamini kukimbilia ndoa kunaweza kuwaweka watoto katika mazingira hatarishi, ikiwamo uwezekano wa manyanyaso au kutelekezwa.
“Ni mapema mno. Watoto wangu ndio kipaumbele. Sitaki waishi maisha ya taabu kwa maamuzi yangu ya haraka,” anasisitiza.
Anaamini kuwa baadhi ya wajane hukimbilia kuolewa wakidhani ni suluhisho la matatizo ya kiuchumi, lakini matokeo yake huwa tofauti.
“Wapo wanaokimbilia ndoa watoto wao wanateseka, wananyanyasika na wengine hujikuta wanaangukia kwenye tabia mbaya. Ni bora mwanamke ajisimamie kwanza mwenyewe,” anasema.
Jioni inapowadia na shughuli za siku kukamilika, Rehema hurudi nyumbani akiwa amechoka, lakini moyoni ana faraja. Anasema huwaangalia watoto wake wakisoma au kucheza, akijua kuwa juhudi zake za kila siku zinaweka msingi wa kesho yao.
Hadithi yake si ya maandazi pekee, bali ni ya uthubutu, kujitambua na mapenzi ya mama kwa watoto wake.
Katika mitaa ya Nonde, harufu ya maandazi yake imekuwa ishara ya mwanzo mpya, uthibitisho kwamba ujane si hukumu ya kushindwa, bali unaweza kuwa hatua ya kuamka na kusimama imara.
Kwa wanawake wengine, hususan wajane, Rehema ana ujumbe mmoja: wasikubali kubweteka au kuishi kwa kuomba msaada kwa kisingizio cha ujane.
Anasema wanapaswa kutafuta fursa, hata kama ni ndogo na wajenge kesho ya familia zao kwa mikono yao wenyewe.
Anasema kwa upande wake maisha yamekuwa darasa. Na kila siku anapoinua beseni lake la maandazi, si tu anauza kitafunwa, bali anauza somo la ujasiri na matumaini kwa majirani na watu wanaomfahamu.