Mwendelezo wa Mgogoro unatokota Mashariki ya Kati unaendelea kuweka shinikizo katika masoko ya kimataifa ya nishati, kufikia sasa wastani wa bei ya mafuta katika soko la dunia imepanda kwa asilimia 13.
Kanda hiyo inachangia sehemu kubwa ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta na gesi duniani. Mvutano wowote wa kijeshi, kisiasa au siasa za ukanda huibua mshtuko kwenye bei za mafuta, mfumo wa ugavi, na gharama za usafirishaji, na athari zake husambaa haraka katika uchumi wa nchi zinazoagiza mafuta, ikiwemo Tanzania.
Katika muktadha huu, umuhimu wa kuwa na hifadhi ya kimkakati ya mafuta (Strategic Petroleum Reserve) ni jambo inayotakiwa kupewa kipaumbele cha sera ya uchumi wa taifa. Kama ambavyo pia Rais Samia alivyogusia kuhusu hilo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta bandari ya Dar es Salaam.
Mambo kadhaa yafuatayo yanaonesha umuhimu wa kuwa na hifadhi ya mafuta ya kimkakati; kwanza ni Uhakika wa nishati, Tanzania ni mwagizaji wa mafuta. Mshtuko katika usambazaji wa kimataifa unaweza kusababisha upungufu wa mafuta ndani ya muda mfupi.
Hifadhi ya kimkakati ni bima ya kurefusha uwezo wa kumudu changamoto hiyo. Lengo la msingi si biashara, ni uthabiti wa dharura. Mataifa makubwa kwa mfano Marekani inakadiriwa kuwa na hifadhi ya taifa ya mafuta inayoweza kufikia mapipa milioni 714, kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Wizara ya Nishati ya Marekani (Us Department of Energy).
Pili ni uthabiti wa bei, upandaji bei ya mafuta kwa mshtuko huongeza mfumuko wa bei unaochochewa na kuongezeka bei za nishati (energy prices). Ikiwa taifa lina hifadhi ya kimkakati, linaweza kuachia sehemu ya akiba wakati wa upungufu wa ghafla ili kupunguza shinikizo la bei za ndani. Hifadhi ya kitaifa inaweza kusaidia kuwa namna ya kudhibiti bei ya mafuta kutopanda kwa kushtukiza kwa haraka wakati wa dharura.
Tatu ni ulinzi wa mizania ya malipo kimataifa, Kwa nchi inayoagiza mafuta, kupanda kwa bei za kimataifa huongeza gharama za uagizaji, kuathiri akiba ya fedha za kigeni, na kulipa zaidi kwenda nje ya nchi.
Hifadhi ya kimkakati hununuliwa kwa utaratibu wa muda mrefu na kwa bei zinazotawanywa (price smoothing), hivyo kupunguza utegemezi wa ununuzi wa dharura katika soko lenye bei ya juu, akiba ya mafuta itasaidia kuepuka kulipa kwa bei ya juu hali inayoongeza nakisi katika mizania ya malipo kwenye biashara ya kimataifa (balance of payment deficits).
Nne ni uthabiti wa shughuli za kiuchumi na kijamii
Mafuta ni pembejeo ya msingi katika usafiri, uzalishaji wa umeme katika baadhi ya mifumo, kilimo, na sekta ya viwanda. Upungufu wa ghafla unaweza kusimamisha shughuli za uzalishaji, kuathiri mapato ya serikali na ajira.
Mataifa kama China na India yamewekeza katika hifadhi za kimkakati ili kulinda uchumi wao unaokua kwa kasi dhidi ya mishtuko ya ghafla ya nje. Hifadhi hizi hutoa muda wa kupanga upya mikataba ya usambazaji bila kusababisha kusimama kwa uzalishaji.
Na tano ni Chombo cha sera ya kimkakati ya muda mrefu, hifadhi ya mafuta si ghala la akiba tu; ni akiba inaweza kutumika wakati wa migogoro ya kikanda, mivutano ya kikanda na nchi kujitosheleza. Katika mazingira ya ushindani wa rasilimali na migogoro ya mara kwa mara, nchi yenye akiba ina nafasi pana zaidi ya kufanya maamuzi ya kimkakati bila shinikizo la haraka la soko.
Uanzishwaji wa hifadhi ya kimkakati ya mafuta unahitaji uwekezaji, miundombinu ya kuhifadhi, na usimamizi. Katika ulimwengu ambapo muktadha wa kibiashara na siasa hubadilika mara kwa mara hifadhi ya kimkakati ya mafuta ni nyenzo ya msingi ya usalama wa uchumi wa taifa.