Masoko makubwa dunia yatikishwa, DSE yaendelea kujidhatiti

Dar es Saalam. Masoko ya hisa duniani yameonesha hali tete na mabadiliko makubwa tangu kuzuka kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran, hatua hiyo huenda ikawa na athari chanya katika masoko ya Afrika endapo hakutakuwa na mdororo wa uchumi wa dunia.

Katika soko la Asia, MSCI Asia Pacific faharisi ilishuka kwa zaidi ya asilimia 2.5, na katika soko kubwa kama la Kospi Korea Kusini ilikuwa kwa asilimia 7.2, Nikkei 225 ya Japani na Hang Seng ya Hong Kong pia walipata hasara kutokana na hofu ya stahili za kiuchumi kutokana na mzozo huo.

Uchambuzi unaonyesha soko la Marekani pia limepitia misukosuko, ambapo hisa kwenye viashiria vikuu kama S&P 500 na Nasdaq zilishuka mara kadhaa baada ya mauaji ya viongozi wa Iran na mashambulizi ya kijeshi kufuatia, huku viashiria vya hatari (VIX) vikiongezeka dalili ya wasiwasi wa wawekezaji.

Masoko ya Ulaya pia yameathirika vibaya. Viashiria kama FTSE 100, DAX na CAC 40 vimeonyesha kushuka kutokana na hatari kubwa za kiuchumi na ukuaji wa uchumi wa dunia huku bei ya mafuta ghafi ikipanda kwa asilimia 13.

Hata hivyo kwa upande wa Tanzania Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Peter Nalitolela alisema athari za mzozo huo bado hazijaonekana katika soko la ndani lakini kuna uwezo mkubwa ukasababisha kupanda au kushuka kwa biashara.

“Kwa kawaida inapotokea misukosuko masoko la mitaji na dhamana huathirika na athari zake zinaweza kuwa za muda mfupi au muda mrefu. Kwa kinachoendelea sasa huenda masoko la Afrika ikiwemo DSE yakanufaika kwani tunatarajia wawekezaji wa Asia watakuwa wanatafuta sehemu salama za kuwekeza,” alisema Nalitolela.

Hata hivyo Nalitolela alisema mgogoro huo kwakuwa unaongeza bei ya mafuta huenda ukasababisha mfumko wa bei kote duniani jambo ambalo linaweza kuathiri uchumi wa dunia na masoko yote hisa.

Hata hivyo pamoja na kuwa imani ya kuendelea kuimarika kwa soko alisema athari chanya au hasi sokoni zitategemea muda ambao mzozo huo utachukua na athari zake katika uchumi mpana wa duniani.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa soko alisema kwa ujumla mtaji wa na ukwasi wa DSE umeendelea kuongezeka jambo ambalo linaonyesha imani ya wawekezaji ambao nao idadi yao sokoni imeongezeka.

Kwa ujumla Nalitolelawa alisema mtaji wa soko hadi Februri 2026 ulifikia Sh34.6 Trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 80.8 ikilinganishwa na mtaji wa Sh19.1 trilioni uliokuwepo kipindi kama hicho mwaka jana.

“Kwa upande wa mauzo katika kipindi cha Februari, 2026 pekee mauzo ya hisa yalikuwa Sh242 bilioni ambayo ni sawa na theluthi moja ya mauzo yote ya mwaka 2025 ambayo yalikuwa Sh663.7 bilioni,” alisema.