Kahama. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ametumia takribani saa tatu kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Phantom mjini Kahama, huku Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), Baraka Msumi akizomewa na wananchi wakati akijibu malalamiko ya huduma za afya.
Kihongosi yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku nne yenye lengo la kufuatilia uhai wa chama, kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na kusikiliza changamoto za wananchi. Katika mkutano huo ulioanza saa tisa alasiri hadi saa 12 jioni, baadhi ya kero zilitolewa na kutatuliwa papo hapo huku nyingine zikiahidiwa kufanyiwa kazi kabla ya kumalizika kwa ziara hiyo Machi 7, 2026.
Moja ya malalamiko makubwa ya wananchi ni upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vya afya, wakidai wagonjwa hulazimika kununua dawa katika maduka binafsi. Akijibu suala hilo, Msumi alisema hadi Februari 28, 2026 upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vya afya ulikuwa umefikia asilimia 89.3, kauli iliyosababisha wananchi kumpinga na kumzomea.
Mwananchi mmoja alidai kuwa katika kituo cha afya alitakiwa kununua sindano tano za kupima malaria kwa mtoto wake wa mwaka mmoja, kila moja ikiwa Sh3,000, baada ya wahudumu kushindwa kupata mshipa mara kadhaa. Baada ya maelezo hayo, DMO alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na Kihongosi akaagiza Sh15,000 alizolipa mwananchi huyo zirudishwe.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akisikiliza kero za wananchi Kahama.
Wananchi pia walilalamikia ubovu wa barabara ya Isaka, changamoto za ardhi, ukusanyaji wa taka, pamoja na kuchelewa kupatikana kwa mita za maji licha ya wananchi kulipia kwa muda mrefu. Kihongosi alimtaka Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Joseph Mkwizu kuanza mara moja ukarabati wa barabara hiyo.
Kuhusu tatizo la mita za maji, Kihongosi alipiga simu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri ambaye aliahidi kulifanyia kazi, huku Kihongosi akisema majibu yatatolewa kabla hajamaliza ziara yake mkoani Shinyanga.
Mbali na kusikiliza kero za wananchi, Kihongosi pia alikagua ujenzi wa bandari kavu na stendi mpya ya Mbulu mjini Kahama, akisema miradi hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na kuonya dhidi ya uwepo wa vishoka katika ugawaji wa vibanda vya biashara pindi ujenzi utakapokamilika.