TANZANIA IMEENDELEA KUIMARISHA USHINDANI WA HAKI ZA UDHIBITI WA BIDHAA BANDIA

Na Maandishi Wetu, Dodoma.

Tanzania inaendelea kuimarisha ushindani wa haki na udhibiti wa bidhaa bandia kupitia Tume ya Ushindani (FCC) pia Sheria ya Alama za Bidhaa, 1963 inalinda biashara halali na watumiaji dhidi ya udanganyifu.

FCC inaidhinisha miungano 4 katika sekta ya fedha, ikilenga kuimarisha mfumo wa malipo ya kidijitali na huduma za benki. Aidha, udhibiti wa bidhaa bandia unaendelea kulinda biashara halali na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC),  Khadija Ngasongwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, leo Machi 05, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Khadija amesema Katika kipindi cha 2025/26, Tume ya Ushindani imeidhinisha miungano 4 katika sekta ya Fedha, Kuidhinishwa kwa miungano hii miwili (2) katika sekta ya fedha na malipo kunaweza kuleta mabadiliko chanya kwa Tanzania kwa kuimarisha mfumo wa kadi na malipo ya kidijitali kupitia uwekezaji wa Toppan Global Security Limited katika DZ Card (Africa) Limited, hivyo kuongeza usalama na ufanisi wa miamala ya kielektroniki.

Vilevile, muungano unaohusu kampuni ya Soren Investment Company Limited na Habib African Bank Limited unatarajiwa kuleta mtaji mpya na uwezo wa kibiashara ili kuimarisha huduma za benki, kutanua upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wananchi, na kuchochea ushindani katika sekta ya fedha ambao unaweza kupunguza gharama za huduma za kifedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu na uwekezaji katika teknolojia za kifedha.

Aidha amesema Udhibiti wa Bidhaa Bandia FCC imeendelea kusimamia kikamilifu Sheria ya Alama za Bidhaa, 1963 ambayo jukumu muhimu katika kuzuia uingizaji, uuzaji, na usambazaji wa bidhaa bandia au zile zenye maelezo potofu. 

“Bidhaa bandia huzuia ushindani wa haki, kuathiri vibaya biashara halali, na kuhadaa watumiaji, hivyo kuunda uwanja usio sawa wa biashara. Sheria hii inahakikisha kuwa biashara zinapewa fursa ya kufanikiwa kutokana na ubora, ubunifu, na kufuata sheria, badala ya udanganyifu”

Hata hivyo amesema hiyo inakuza soko lenye ushindani wa haki na uwazi, likilinda imani ya watumiaji na kuwezesha makampuni kuwekeza kwa kujiamini katika ukuaji na ubunifu.

Kudhibiti bidhaa bandia kwa mujibu wa sheria hii pia kunachangia ukuaji wa uchumi. Biashara halali zinabaki na mapato yao, jambo linalochochea uwekezaji zaidi, kuongeza ajira, na kuendeleza ubunifu. Watumiaji wanalindwa dhidi ya bidhaa zisizo salama au zisizo halisi, na hivyo kupunguza hasara za kiuchumi zinazotokana na udanganyifu. 

Aidha, jitihada za kuzuia bidhaa bandia zinaboresha sifa ya biashara kitaifa na kimataifa, kuwavutia wawekezaji, na kuongeza mauzo ya nje, Kwa kuunganisha utekelezaji madhubuti, ushirikiano wa sekta, na uhamasishaji wa Umma, Sheria hiyo inahakikisha kuwa ushindani wa haki na uthabiti wa kisheria unachochea ukuaji wa uchumi endelevu wa nchi.