Willium Edgar atamani kuifunika rekodi yake ya msimu uliopita

MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Edgar William amesema licha ya kiwango kizuri anachoendelea kukionyesha kwa sasa akiwa na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, lakini malengo yake makubwa ni kufunga mabao mengi zaidi ya aliyoyafunga msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Edgar aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Fountain Gate, alisema mwenendo wake mzuri unampa motisha ya kuzidi kupambana zaidi, ingawa malengo yake ni kuivuka rekodi yake aliyoiweka msimu uliopita.

“Mchezaji mzuri ni yule anayevuka malengo aliyoweka msimu uliopita, kwa sasa niko katika mstari mzuri, ingawa bado nina kazi kubwa ya kuhakikisha natimiza hilo, jambo nzuri kwangu ni kuona naaminiwa na benchi letu la ufundi,” alisema Edgar.

Kabla ya kutua Dodoma Jiji, msimu wa 2024-2025, Edgar aliifungia Fountain mabao sita ya Ligi Kuu na kuasisti pia mawili, huku akikumbukwa msimu wa 2023-2024, alipokuwa mfungaji bora wa Championship akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21.

Mbali na ufungaji bora, Edgar alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Championship msimu wa 2023-2024, akiwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye akiwa na kikosi cha KenGold na Mganda Boban Zirintusa, ambaye alikuwa akichezea Biashara United.

Nyota huyo anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amepandisha timu mbili Ligi Kuu Bara, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha KenGold msimu wa 2023-2024.

Kwa msimu huu, mshambuliaji huyo amefunga mabao matano ya Ligi Kuu, akibakisha bao moja tu kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, akizidiwa na Salehe Karabaka wa JKT Tanzania mwenye sita na kinara, Fabrice Ngoy wa Namungo aliyefunga manane.