Simulizi za wazazi malezi ya watoto njiti

Dar es Salaam. Kwa wazazi wa watoto njiti, kila pumzi ya mtoto ni ushindi na kila usiku wa hofu ni hatua nyingine kuelekea kwenye mwanga wa kesho.

Mohammed Salim anakumbuka siku ya Mei 5, 2017 ambayo maisha yake na ya mkewe yalibadilika kwani wakati wao wakiwa wamejiandaa kupata mtoto wa pili, safari yao iligeuka kuwa vita vya uhai na kifo wa mtoto wao.

Anakumbuka tarehe hiyo kama siku ya kawaida ambayo mke wake alimuambia hajisikii vizuri na apelekwe hospitalini, baada ya vipimo daktari alimwita na kumwambia hali ya mtoto wanayemtarajia si nzuri kwani maji tumboni yamekauka na kitovu kimeanza kujifunga shingoni.

Hivyo alitakiwa kufanya upasuaji wa dharura ili kumnusuru mama jambo lililowalazimu kukubaliana na hali halisi licha ya kutojiandaa kwa chochote walipotoka nyumbani, kwani walidhani wanakwenda na kurudi.

Baada ya muda kupita mkewe akiwa chumba cha upasuaji, ghafla alisikia sauti ikimwita na kumpongeza kuwa mke wake amejifungua salama lakini mtoto wao alikuwa njiti, mwenye uzito wa Kg1.3 pekee.

“Sikuwahi kusikia kuhusu watoto njiti hapo kabla wala kumuona, sikuwahi kumsikia ndugu yangu yoyote akiwa na mtoto huyo ndipo nilianza kusikia habari za kutisha kuwa watoto wale hawakui wengi hupoteza maisha,” amesema.

Amesema simulizi hizo zilimfanya kuwa makini zaidi katika kuhakikisha anamhudumia mwanaye kwa kiwango kinachotakiwa huku akijifunza zaidi kuhusu malezi na makuzi yao,  lakini kuna wakati alilazimika kuamka usiku kuangalia kama mtoto bado anapumua.

Amesema katika safari ya malezi ya mtoto huyo, waliporuhusiwa kurudi nyumbani walihakikisha kwa miezi minne ya kwanza mtoto haguswi na maji walimfuta futa mwilini kwa mafuta ya nazi na mzeituni.

“Hakuna ndugu, jamaa wala rafiki aliyeruhusiwa kumshika, hata dada wa kazi hakuruhusiwa kumuona. Mke wangu alipambana sana kumnyonyesha,” anasema Mohammed.

Anasema katika kipindi cha mwezi mmoja pekee cha kuhudumia mtoto huyo wakiwa nyumbani walipokwenda kliniki daktari alishangaa kuona mtoto alipanda kutoka kilo 1.3 hadi kilo tatu.

“Hapo ndipo nikaanza kuamini kwamba ataishi.”

Lakini changamoto hazikuishia hapo, Mohammed anasema mtoto alizaliwa na mashimo mawili kwenye moyo walilazimika pia kuhudhuria kliniki katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

“Baada ya miezi sita, shimo moja lilifunga na jingine likapungua taratibu na hadi sasa mtoto yuko salama.

Miaka miwili baadaye familia ya mohammed ilibarikiwa tena kupata mtoto njiti wa pili, lakini anakiri kuwa safari ya kwanza ilikuwa imemfundisha hivyo walijiandaa mapema.

“Alikuwa na kilo 1.4 pekee…. safari hii tulihakikisha mtoto ana bima ya afya. Tulifahamu ni gharama kubwa, lakini tulikuwa tumejifunza namna ya kupambana,” anasema Mohammed.

Leo, mtoto wao wa kwanza yuko darasa la nne akiwa na miaka minane, ingawa ukuaji wake ni tofauti na watoto wa kawaida lakini anao uwezo mkubwa kiufahamu kiasi cha shule kumrusha darasa moja.

“katika safari ya malezi ya mtoto njiti wa kwanza, biashara yetu ya shule ya Day care ilikufa kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu iliyokuwa ikisimamiwa na mke wangu, biashara yangu ya usambazaji vifaa vya kompyuta katika shule ilikufa kutokana na kukosa muda, hivi sasa ndiyo tumeanza upya,” amesema.

Lakini si Mohammed pekee aliyeishi simulizi hii, Mary Marwa mama wa mtoto njiti aitwaye Aaron ana kumbukumbu za maumivu ya uzazi ambayo hayatasahaulika.

Akikiri kuwa kipindi cha mwanzo cha mimba alikuwa akipitia maumivu wakati wa usiku lakini kila asubuhi alipoamka alihisi yuko sawa na kwenda kazini.

Hali hiyo ilipoendelea, alilazimika kwenda kufanya vipimo vyote ambapo majibu yalionyesha yupo sawa jambo lililomfanya kuendelea na kliniki ya ujauzito kama kawaida.

“Majibu kuwa nipo sawa ilihali ninaumwa ndiyo yaliyonifanya nihame kliniki na kuanza upya katika Hospitali ya Lugalo.”

Akiwa anaendelea na kliniki hospitalini hapo aliwaeleza kuwa anasikia maumivu kwenye kibofu ndipo alifanyiwa vipimo na kuambiwa kuwa ana protini nyingi katika mkojo, huku wakimpa sharti la kupima shinikizo la damu kila siku.

“Kila siku niliyokuwa naenda kupima shinikizo la damu lilikuwa juu kuliko siku mbili nyuma, hali hiyo ilinifanya kuhamia katika hospitali kubwa zaidi jijini hapa na nilipofanyiwa vipimo niliambiwa figo na ini zilikuwa hazifanyi kazi vizuri ndiyo maana nilikuwa na protini nyingi kwenye mkojo,” anasema.

Amesema kutokana na hali aliyokuwa nayo mimba yake ikiwa na wiki 24 alishauriwa aitoe kwani hali ikiendelea hivyo angeweza kupooza au kupata kichaa cha mimba na hata mtoto wa umri huo angezaliwa angekuwa na tundu kwenye moyo, kichwa kikubwa au mapungufu.

Hata hivyo alipopata ugumu katika kusaini nyaraka za kukubali kutoa mimba hiyo, ndipo muujiza ulipotokea kwani baada ya mahangaiko alifanikiwa kujifungua, wauguzi walidhani mtoto amefariki na kumuweka sehemu ya uchafu.

Muuguzi mmoja aliona yule mtoto aliye katika eneo la takataka kuwa mzima alimchukua na kumpeleka wodini alipomtekenya alilia na hata alioambiwa kuwa wazazi walisaini hati ya kutoa mimba lakini aligoma kumtupa.

“Mtoto huyo alizaliwa na gram 600. Baada ya siku nne walipoona anaendelea kuishi walimuhamishia kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU) alipewa uangalizi mzuri, hakuwahi kupunguza uzito tangu hapo.  Ndani ya siku tatu angalau akaongezeka na kufikia gramu 10 akiongezeka 30 inakuwa ni sherehe, tulikaa hospitali miezi mitatu na tulitoka akiwa na kilo 1.2 na kutokana na gharama kuendelea kupanda nililizimika kujifunza kila kinachofanyika ili niruhusiwe kurudi nyumbani,” anasema.

Anasema walipoona amejua namna ya kumuhudumia mtoto aliruhusiwa kutoka na alipofika nyumbani ndani ya siku tatu mtoto aliongeza gram 300. Kwa kipindi hicho hakuruhusiwa kumnyonyesha hadi pale alipofikisha umri wa miezi tisa ambao angepaswa kuzaliwa.

Wakati huo bima ilikuwa hailipii watoto njiti hivyo gharama zote zilikuwa juu ya wazazi na hadi wanatoka hospitalini bili yao ilikuwa zaidi ya Sh50 milioni.

Katika safari hii, Mary alijikuta akipoteza ajira yake ya ualimu kutokana na kutumia muda mrefu kuhudumia mtoto hata miezi mitatu ya uzazi ilipokwisha.

Abdallah Issa ambaye pia ni baba wa pacha njiti waliowapata mwaka jana, naye ni miongoni wa waliobeba alama ya safari hii.

Watoto wao walizaliwa na wiki 26 pekee, wakiwa na uzito wa gramu 800 kila mmoja ikiwa ni muda mchache tangu madaktari wapendekeze mimba hiyo itolewe ili kumnusuru mama, kwani uwezekano wa watoto kupona ulikuwa mdogo.

Watoto hao waliozaliwa kwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuzaliwa walihamishiwa katika chumba cha uangalizi maalumu cha watoto wachanga (NICU), ambapo gharama zilikuwa Sh1 milioni kwa siku kwa watoto wawili.

“Hatukuwa na uhakika kesho itakuwaje. Tulikaa hospitalini kwa miezi mitatu baadaye tuliruhusiwa wakiwa na uzito wa kilo 1.5 kila mmoja. Leo, wakiwa na miezi tisa, wana uzito wa kilo sita wa kike anatambaa wa kiume anakaa, wanacheka na wanaonesha uhai ambao ulionekana hauwezekani,” amesema.

Wazazi hawa wanapendekeza Serikali iangalie namna ambayo inaweza kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya watoto njiti, kwani gharama za kuwahudumiwa ni kubwa ambazo zinaweza kufanya wazazi wengi kukata tamaa.

Akielezea ni hatua gani inayoweza kufanya madaktari kupendekeza mimba itolewe kwa ajili ya kumnusuru mama, Daktari wa kinamama, Cyrill Massawe anasema ni magonjwa ya figo na saratani.

“Kama figo hazifanyi kazi inavyotakiwa inaweza kushauriwa mimba itolewe, saratani pia ikiwa katika hatua za kuanza matibabu ya haraka wanakupa ushauri huu hasa kama mimba ikiwa bado itahitaji muda mrefu,”

Anasema kwa mama mwenye saratani ikiwa mimba yake iko mwishoni inaweza kuvumiliwa kwani matibabu ya saratani ikiwemo mionzi haiendani na ukuaji wa mtoto.

Mbali na kutolewa kwa mimba, Dk Massawe anasema mtoto kwa kawaida anatakiwa kukaa tumboni wiki zisizopunguza 38 ili azaliwe wakati ambao mifumo yake yote inayoweza kumsaidia kuishi ikiwa kamili.

Inapotokea anazaliwa kabla ya wakati, inaweza kuwa ngumu kupona kulingana na kiwango cha ukomavu wa mifumo yake.

“Baadhi wanaoishi ni wale ambao wanakuwa amekomaa mifumo kiasi hivyo hata akipewa msaada kama wa upumuaji inakuwa ni kwa muda mfupi,” anasema.

Akielezea kwa nini baadhi ya kinamama hupata watoto njiti, Dk Massawe anasema hakuna sababu maalumu, ingawa kuna magonjwa huchangia hilo.

“Presha wakati wa ujauzito, kisukari, maambukizi ya ugonjwa kama malaria magonjwa ya mfumo wa hewa, wengine njia inafunguka kabla ya wakati lakini zipo na sababu nyingine zinazoweza kusababisha hali hili,” anasema.