Sikia hii ya Mwangosi Simba

MSHAMBULIAJI wa Simba, Baraka Mwangosi ametajwa kama mchezaji atakayefanya makubwa baadaye, huku akitakiwa hivi sasa kujifunza vitu vingi kiufundi na ushindani vitakavyomjengea kujiamini na kutegemewa katika timu hiyo na Taifa Stars.

Miongoni mwa walioliona hilo ni staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel aliyesema Mwangosi anatakiwa kupewa muda kupata uzoefu, kujifunza vitu vingi katika timu, jambo litakalomjenga na kuwa mchezaji bora.

“Mwangosi ana kipaji kikubwa, ili kionekane kinatakiwa kuvumiliwa, kadri anavyoendelea kuyasoma mazingira ya Simba ambayo ni tofauti na Mbeya City alikotoka mbeleni atakuwa tegemeo, si Simba tu bali hata timu ya taifa ya Tanzania,” alisema Gabriel na kuongeza;

“Ana kipaji kikubwa kinachotakiwa kuongezewa ufundi wa makocha, jambo la msingi kwa Mwangosi awe mtu wa kupenda kujifunza kwa wale ambao ni panga pangua kikosini, ajitume kwa bidii katika mazoezi ya timu na binafsi, hilo litamsaidia Watanzania kukiona kipaji chake.”

Aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alisema: “Dogo ana kipaji kikubwa, anachotakiwa ni kupambana na kuendelea kujifunza mbele ya waliyomzidi uzoefu, lakini naamini siku za usoni atafanya makubwa na awe na muendelezo wa kiwango cha juu.”

Mshambuliaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Marcel Kaheza alisema: “Mchezaji yoyote anayesajiliwa Simba au Yanga anakuwa na kitu kikubwa, ili kuendelea kusalia katika klabu hizo, lazima kujituma na kupambana kwa bidii, kwa sababu zinasajili wachezaji wenye vipaji vikubwa ndani na nje.”

Kaheza aliongeza: “Nimeichezea Simba nikitokea Majimaji kipindi hicho jina langu lilikuwa juu, lakini kulikuwa na ushindani mkali, ninachosisitiza Mwangosi akaze buti, kujiunga Simba ni hatua moja, kuaminiwa kikosi cha kwanza ni jambo lingine hapo ni bidii yake ndiyo itakayombeba pia ajue katika nafasi yake kila mmoja anataka kucheza, hivyo azidishe ushindani wa kumshawishi kocha na asijichukulie mchezaji wa kawaida.

“Mfano wakati Simba inatangaza kumsajili beki wa kushoto, Nickson Kibabage wengi waliona amekosea njia, ila bidii yake ndiyo inayorejesha heshima mbele ya mashabiki wa timu hiyo, vivyo hivyo kwa Mwangosi anapaswa asijione ni mchezaji wa kawaida.”