Planet, Bandari kazi ipo fainali Dunda Swish Basketball Tournament

FAINALI ya kwanza ya Dunda Swish Basketball Tournament,  inatarajia kufanyika keshokutwa (Jumapili) ikizikutanisha Bugando Planet na Bandari Mwanza, kwenye Uwanja wa Mirongo, Mwanza.

Fainali hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo, itachezwa kwa mfumo wa kucheza michezo mitatu ‘best of three play off’ na ubora wa timu hizo unachangia mvuto.

Endapo timu moja itashinda mechi mbili (2-0), itatangazwa bingwa wa mashindano.

Planet ilifuzu fainali baada ya kuifunga timu ngumu ya Mwanza Eagles katika nusu fainali ya michezo mitatu ya  ‘best of three play off’ na ilishinda 2-1, huku nusu fainali ya kwanza ikipata pointi 69-56, ya pili Eagles ikashinda 80-63, na ya tatu Planet ikashinda 70-67.

Katika nusu fainali hiyo, John Sapa wa Planet alifunga pointi 19, kupokonya mipira (Steal) mara mbili, alidaka (rebound) nne na asisti mbili.

Sapa ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo, alisema timu yao inatumia mfumo wa kucheza wa kitimu na siyo ya kumtegemea  mchezaji mmoja  au wawili.

“Nimeona timu nyingi wanatumia mchezaji mmoja au wawili, endapo wachezaji hao wanakabwa, timu inashindwa  kupata matokeo mazuri,” alisema Sapa na kuongeza, wamejipanga vizuri kutetea kombe hilo walilolibeba miaka miwili iliyopita. 

Bandari Mwanza ilitinga fainali baada ya kuifunga Mwanza Octopus kwa michezo 2-1, huku nusu fainali ya kwanza Octopus ilishinda kwa pointi 85-75, ya pili na ya tatu, Bandari ilishinda  73-51 na 77-57.

Katika nusu fainali hiyo, Zakayo Joseph wa Bandari Mwanza, aliongoza kwa kufunga pointi 19, kupokonya mipira (Steal) mara mbili, alidaka (rebound) nane, alizuia (block) mbili na asisti mbili.

Nyota wa Bandari, Alphoce Kasekwa alitamba timu yake itaivua ubingwa Planet  katika fainali hizo.

“Sisi tuko vizuri, nachosema Bugando Planet wasitegemee mchezo wa kesho kutwa  kuwa mwepesi kwao,”alisema Kasekwa.