Pwani. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Rahma Kisuo ameziagiza menejimenti za viwanda mkoani Pwani kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa endelevu na wenye tija.
Kisuo ametoa agizo hilo Machi 4, 2026 wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi, ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, katika maeneo mbalimbali ya kazi wilayani Kibaha mkoani humo.
Akizungumza katika viwanda alivyotembelea kwa nyakati tofauti, Kisuo amesema licha ya viwanda hivyo kufanya vizuri katika uzalishaji na utekelezaji wa baadhi ya sheria za kazi, bado ziara hiyo imebaini kasoro ndogondogo zinazohitaji kufanyiwa marekebisho.
“Tumetembelea baadhi ya maeneo katika viwanda hivi na kujionea hali ilivyo. Kwa ujumla wanafanya vizuri, ingawa kuna dosari chache tulizobaini, ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kutokuwa na mikataba ya ajira pamoja na kutokidhi baadhi ya viwango vya usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Kisuo.
Kutokana na hali hiyo, amewaagiza watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mamlaka nyingine za udhibiti kutenga muda maalumu wa kufanya ukaguzi wa kina katika viwanda hivyo ili kuwashauri wawekezaji kuhusu maboresho yanayohitajika.
Pamoja na maelekezo hayo, Naibu Waziri huyo amewapongeza wamiliki wa viwanda vilivyotembelewa kwa mchango wao katika kukuza uchumi wa nchi kupitia ulipaji wa kodi pamoja na kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), Khadija Mwenda, ambaye aliambatana na Naibu Waziri katika ziara hiyo, amesema ukaguzi wa awali umebaini upungufu kadhaa katika mifumo ya usalama na afya ya viwanda hivyo.
Amesema baadhi ya changamoto zilizobainika ni pamoja na mazingira ya kazi yenye joto kali, vumbi la makaa ya mawe kutapakaa katika mazingira ya kazi, upungufu wa vifaa vya kinga kwa wafanyakazi na ukosefu wa alama za usalama katika baadhi ya maeneo ya uzalishaji.
Mwenda amemhakikishia Naibu Waziri, wataalamu wa Osha kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watafanya ukaguzi wa kina ili kuwasaidia wawekezaji kupata ushauri wa kitaalamu, utakaowawezesha kuboresha mazingira ya uzalishaji na usalama wa wafanyakazi.
Wakati huohuo, viongozi wa viwanda vilivyotembelewa, akiwemo Msimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa kiwanda cha uundaji magari cha GF Vehicle Assemblies Ltd, Jacob Lerise wamemshukuru Naibu Waziri pamoja na timu yake kwa ziara hiyo na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.
Ziara hiyo ya siku mbili wilayani Kibaha mkoani Pwani ilihusisha ukaguzi katika kiwanda cha bidhaa za usafi cha Keds Tanzania Co. Ltd, kiwanda cha utengenezaji wa trela za malori cha Aluminium Trailers Ltd, kiwanda cha uundaji magari cha GF Vehicle Assemblies Ltd pamoja na kiwanda cha sabuni na vipodozi cha Creative Intertraders Ltd.