Dar es Salaam. Kama Machi Mosi, 2026 ulisikia tangazo la kulipiwa mahari na umejipanga na mwenza wako, basi huna budi kufahamu masharti 10 yaliyotangazwa na Taasisi ya Al-Hikma ili kutimiza kigezo cha kufanikisha mchakato huo.
Miongoni mwa masharti hayo yaliyotangazwa na mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Nurdin Kishki ni pamoja na mwanamke ndio akachukue fomu ya mchakato huo, awe Mtanzania, muombaji asiwe na mume na huyo mtarajiwa wake asiwe na mke.
Mengine ni awe ameposwa na kukubaliwa, mwanaume awe na chanzo cha kupata riziki, awe amejaza fomu na kupita kwenye usaili, awe tayari kufunga ndoa ya pamoja, athibitishwe na imamu wa eneo lake kwa barua na kitambulisho cha Taifa na mzazi wa mwanamke akubali ndoa hiyo itafungwa pamoja na wengine.
Sheikh Kishki ametoa utaratibu huo leo Alhamisi Machi 5, 2026 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu mashindano ya Quran yaliyofanyika Machi Mosi, sambamba na kutoa shukurani kwa watu waliojitolea kufanikisha mchakato huo.
Utaratibu wa kulipia mahari ulitangazwa na Sheikh Kishki siku ya kilele cha mashindano ya mabara ya kuhifadhi Quran tukufu yaliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo vijana 130 watalipiwa mahari.
“Tunajua wanaume wengi wana wachumba, lakini wanawawekea usiku wanawake ambao wakiwaambia waoane wanajibiwa kuwa mambo magumu hivyo wasubirie.”
“Sasa safari hii tumekuja kivingine, mwanamke ndiye aombe fomu kisha akamjuze huyo mumewe mtarajiwa. Ndio mjue kuwa wanawake wana hasira tayari wameshafika ofisini kwa ajili ya fomu,” amesema Sheikh Kishki.
Sheikh Kishki amefafanua mchakato huo hautawahusu wanaotaka kuongeza mke bali wale wanaoingia kwenye ndoa kwa mara ya kwanza ndio watakaozingatiwa, huku akiwaonya wanaume watakaokurupuka kuingia kutaka kuoa pasipo kuwa na shughuli za kuwaingizia kipato.
“Ni muhimu mwanaume kupita kwenye usaili, maana tulishajifunza huko nyuma kuna wengine madishi yameyumba, sasa tunataka kuwaona je, mtambo au sio mitambo,” ameeleza Sheikh Kishki.
Katika mkutano huo, taasisi hiyo imetoa zawadi mbalimbali ikiwemo tiketi za kwenda Makka (Saudi Arabia) kutekeleza ibada ya Umrah, simu za mkononi na fedha taslimu kwa kutambua mchango uliofanywa na watu waliojitolea kufanikisha mashindano hayo wakiwemo wanahabari.
Mmoja ya watu walioshinda nafasi ya kwanza kwa kujitolea kufanikisha mchakato huo ni pamoja na Snura Mushi ambaye amepata zawadi ya tiketi mbili za kwenda Umrah yeye pamoja na mumewe.
“Nina furaha sana hadi nguvu zimeisha, kwa mara kwanza nimeingiza timu Al-Hikma Foundation, siamini kama utendaji wetu umetuwezesha kushika nafasi ya kwanza. Najisikia faraja sana kuona nimefanya kazi kubwa pamoja na timu yangu,”
“Nashukuru kwa zawadi hii hamjanifikiria mimi tu, bali na mume wangu nawashukuru sana kwa mara nyingine,” amesema Snura.