Masaju ataka taasisi za haki jinai ziwajibike, zizingatie Katiba na sheria

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju ameagiza kila taasisi zilizopo katika mnyororo wa utoaji wa haki kuwajibika ipasavyo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi yanayosimamia taasisi husika.

Pia, amesema wadau wa haki wanapaswa kulinda na kuheshimu hadhi ya Mahakama, huku Mahakama nayo ikisimamia kanuni na sheria zilizopo, ikiwemo sheria ya kosa la kuidharau Mahakama.

Jaji Masaju ameyasema hayo Jumatatu Machi 2, 2026, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa mwaka wa wadau wa haki jinai uliofanyika jijini Dodoma.

“Mahakama na wadau wa mnyororo wa utoaji wa haki waimarishe mawasiliano miongoni mwao kwa lengo la kuchukua hatua kwa haraka pale changamoto za utoaji wa haki zitakapojitokeza,” amesema.

Mbali na hayo, Jaji Mkuu huyo ametaka Mahakama na wadau wake kutambua nafasi ya kila mmoja, kudumisha heshima na nidhamu na kuzingatia sheria na taratibu zinazoongoza majukumu yao.

Mkakati mwingine alioelekeza utekelezwe ni kwa kila taasisi inayoshiriki katika utoaji wa haki, kuimarisha ufuatiliaji wa mashauri na uwajibikaji kwa kutoa taarifa sahihi na za mara kwa mara, pamoja na kutumia mifumo inayosomana ili kurahisisha mawasiliano.

“Kila taasisi ambayo ni mdau wa utoaji haki mahakamani iweke utaratibu wa ndani utakaowezesha utekelezaji wa mikakati hiyo,” amesema.

Akizungumza kuhusu maana ya haki, Masaju amesema ni uamuzi unaofanywa na Mahakama kwa kuzingatia na kutekeleza masharti ya Katiba na sheria kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

“Kwa maana hiyo, taasisi zinazohusika zinapokusanya ushahidi zinapaswa kuhakikisha ushahidi huo unatosheleza ili kesi iende mahakamani. Mahakama inapofanya maamuzi, kama mtu hakuridhika ana haki ya kukata rufaa,” amesema.

Jana Jumatano, Machi 4, 2026, baada ya uapisho wa mahakimu jijini Dodoma, Jaji Masaju aliwataka kuzingatia na kuheshimu mila na desturi kama ambavyo Katiba ya nchi inazitambua.

“Katiba inatambua mila na desturi za Tanzania pamoja na viapo. Ndiyo maana tuna Mahakama zinazotambua mila na desturi hizo. Mahakama za Mwanzo, mnapotekeleza majukumu yenu katika mashauri yasiyo ya jinai, zingatieni mila, desturi na sheria za Kiislamu,” amesisitiza.

Ameongeza si lazima mtu kufanya kazi katika eneo alikozaliwa, kwani wapo watakaokwenda kufanya kazi mijini au vijijini. Hivyo ni muhimu kutambua mila na desturi za maeneo husika ili kusaidia kutatua migogoro inayohusiana na masuala hayo kwa haki.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Dk Mustapher Siyani, amewataka mahakimu nchini kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa bila kuzingatia nguzo hizo haki haiwezi kutendeka kwa ufanisi.

Amesema kazi ya hakimu si ya mazoea bali ni dhamana kubwa kwa umma inayohitaji mtu mwenye maadili thabiti na uwezo wa kitaaluma.

“Sasa mambo haya yanabeba msingi kwa kazi mnayoenda kuifanya. Mtumishi yeyote wa Mahakama au wa umma, hususani hakimu au jaji, anapaswa kuyachukua na kuyazingatia mambo haya matatu kama sehemu ya maisha yake.