Nsajigwa aanza na pointi moja Prisons, Ibenge akunja sura

Wakati Azam FC ikinung’unika na sare ya pili mfululizo, Tanzania Prisons ni kicheko kwa kupata pointi moja dhidi ya wapinzani wao hao katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kabla ya mechi hiyo iliyopigwa leo Machi 5, 2026 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Azam ilitoka kupata pointi moja kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Pamba Jiji huku Prisons ikilala 2-0 kwa Simba.

Mechi hiyo ilikuwa wa kwanza kwa Kocha Shadrack Nsajigwa tangu kutambulishwa Tanzania Prisons akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Zedekiah Otieno raia wa Kenya.

Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa tahadhari na mashambulizi ya kushtukiza lakini ilishuhudiwa dakika 45 za kwanza zikiisha kwa nguvu sawa bila kufungana.

Hata hivyo, Azam itajilaumu zaidi kufuatia nafasi za mipira ya kutenga kutoitumia vyema baada ya mashuti yote kutokuwa na madhara langoni mwa Prisons.

Kipindi cha pili, Azam ilionekana kutawala mechi kwa mashambulizi ya mara kwa mara, huku Prisons ikifanya jukumu la kuokoa zaidi hatari haswa kipa wake Mussa Mbisa aliyesimama imara golini.

Dakika ya 77, Prisons iliamua kufanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumpumzisha Lambart Sabiyanka aliyempisha Samson Mbangula na Never Kagoma akichukua nafasi ya George Mpole.

Mabadiliko hayo yaliipa nguvu Maafande hao haswa eneo la ushambuliaji ambapo Mbangula aliweza kuwapa ugumu mabeki kwa kosa kosa dhidi ya kipa Aish Manula ikiwamo dakika 90 walipomkosa kipa huyo kwa kuokoa shuti la Never.

Azam pia ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Zidane Sereri na nafasi yake kujazwa na Albogast Kyobya huku James Akaminko akimpisha Sadio Kanoute, lakini ubao ukabaki vilevile.

Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge, amesema sare hiyo si matokeo mazuri kwao baada ya kupata matokeo kama hayo dhidi ya Pamba Jiji akieleza kuwa bado hawajakata tamaa kwakuwa Ligi haijaisha.

Amesema walikuwa na matarajio ya ushindi kutokana na maandalizi lakini nyota wake walipambana wakakosa umakini wa kutumia nafasi za mabao walizopata.

“Si matokeo mazuri kwetu kwakuwa tuliumudu mchezo lakini licha ya jitihada za wachezaji ila hawakuweza kutumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao, nitalifanyia kazi kwa mechi zijazo,” amesema Ibenge.

Kocha Mkuu wa Prisons, Shedrack Nsajigwa, amesema pointi moja kwao si mbaya hapo kuwa walihitaji ushindi akikiri kuwa bado wanao wakati mgumu kupambana kila mechi.

“Uwanja pia haukuwa mzuri lakini nishukuru kwa matokeo haya kutokana na ugumu wa Azam na ubora wao, tunaenda kujipanga kwa mechi zijazo,” amesema Nsajigwa.