::::::::
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imemfikisha mahakamani Askofu Renatzs Joseph Nyalali wa kanisa la Hosanna Assemblies of God (HAOGT).
Anakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka na kutoa taarifa za uongo kuhusu umiliki wa ardhi.
Inadaiwa alifanya hivyo ili kujipatia kiwanja kinachodaiwa kuwa na thamani ya Sh milioni 60.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Ismail Bukuku, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya taasisi hiyo kupokea malalamiko kutoka kwa mmoja wa warithi wa marehemu Ally Hamaf Hillal.
Bukuku amesema mlalamikaji huyo pia ni msimamizi wa mirathi ya marehemu huyo.
Amesema uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwepo kwa tuhuma za kughushi nyaraka zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Kwa mujibu wa mashtaka, tukio hilo linadaiwa kutokea kati ya mwaka 2021 na 2022.
Inadaiwa mshatakiwa alighushi nyaraka zinazodaiwa kuwa za wanafamilia wa marehemu.
Lengo likiwa kujipatia umiliki wa eneo la ardhi lililopo Mtaa wa Kizani, Gezaulole, wilayani Kigamboni.
Eneo hilo linadaiwa kununuliwa mwaka 2008 na marehemu Ally Hamaf Hillal.







