Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema mkoa wa Dar es Salaam bado unaongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.
Amesema hali hiyo inachangiwa zaidi na msongamano mkubwa wa watu pamoja na muingiliano wa shughuli nyingi za kiuchumi.
Henga ametoa kauli hiyo wakati wa warsha ya kutathimini ukatili wa kijinsia kwa wanawake katika sekta ya afya iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha ukatili wa kijinsia bado ni kikubwa nchini, huku wanawake wakiwa waathirika wakuu wa vitendo hivyo katika jamii.
“Kwa ujumla wanawake saba kati ya 10 hukumbana na ukatili wa kijinsia. Ukichukua manusura 10, saba ni wanawake,” amesema Henga wakati akielezea ukubwa wa tatizo hilo.
Ameongeza kuwa ukatili huo huwakumba zaidi wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49, na hujumuisha vipigo, ukatili kutoka kwa wenza, mauaji ya wenza pamoja na ukatili wa kiuchumi unaochangiwa na kipato duni cha wanawake.
Akifafanua zaidi, amesema ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa Dar es Salaam inaongoza kwa matukio hayo kutokana na idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za kiuchumi, huku mikoa ya Tabora na Mara ikifuatia.
Aidha, LHRC imesisitiza umuhimu wa vituo vya huduma ya pamoja (One Stop Centers) kama kile cha Mwananyamala ambavyo husaidia kuhifadhi ushahidi na kumwezesha mhanga kupata haki kwa haraka. Amesema kwa sasa vituo 18 vilivyopo nchini vinakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa watumishi kutokana na uhamisho, hali iliyosababisha kutolewa kwa mafunzo mapya kwa watumishi wa hospitali.











