Kahama. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, ametumia zaidi ya saa tatu kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), Baraka Msumi, akijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na zomea-zomea la wananchi.
Kihongosi yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku nne ikilenga kufuatilia uhai wa chama, kukagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali imepeleka fedha na kusikiliza changamoto za wananchi.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Phantom mjini hapa, Kihongosi alitumia saa tatu kusikiliza kero za wananchi, baadhi zikitatuliwa papo hapo, huku nyingine akizipokea na kueleza kuzifanyia kazi kabla hajaondoka mkoani Shinyanga, Machi 7, 2026.
Miongoni mwa kero walizotoa wananchi ni changamoto ya upatikanaji wa dawa katika maduka ya hospitali na vituo vya afya, wakihoji ni kwa nini dawa hazipatikani na wagonjwa kutakiwa wakazinunue duka la nje.
Katika kero hiyo, Kihongosi alimuita Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), Baraka Msumi, na kumtaka aitolee ufafanuzi ambapo alisema kuwa upande wa hospitali na vituo vya afya hadi Februari 28, 2026, upatikanaji wa dawa ulikuwa asilimia 89.3.
“Katika dawa huwa kuna mwezi wa kutoa ripoti na mwezi wa kupokea dawa, yawezekana kinachozungumzwa ni kipindi cha kutoa ripoti,” amesema Mganga Mkuu wa Wilaya, huku wananchi wakipaza sauti na wengine kuzomea wakidai DMO ni muongo.
Kihongosi ametaka mwananchi anayetaka kusema ukweli wa hilo ajitokeze, mmoja aliyepewa nafasi amesema pamoja na changamoto ya upatikanaji wa dawa, pia kuna changamoto ya kununua sindano ya kupima malaria kwa mtoto.
Ameeleza namna ambavyo mtoto wake wa mwaka mmoja alivyotakiwa kununua sindano tano, kila moja ikiuzwa Sh3,000.
“Mtoto mdogo anapopimwa malaria, mishipa yake haipatikani. Wakiendelea kumchoma sindano ya kwanza, hawajapata mishipa wanakwambiwa imeharibika, ununue nyingine, huku wakiendelea kumchoma choma hadi watakapopata mshipa. Hizo zinazoharibika unaambiwa uzilipie.
“Mwanangu alichomwa mara tano nikaambiwa nilipe Sh15,000, hii si sawa,” amedai mwananchi huyo kabla ya mganga mkuu wa wilaya kukiri kuwepo na ukweli wa hilo, huku Kihongosi akihoji kuhusu sera ya afya kwa mtoto chini ya miaka mitano.
DMO amedai kuna baadhi ya mambo wananchi hawayaelewi, na Kihongosi kumtaka awaelimishe, kwani yeye ndiye mwenye wajibu wa kuwasaidia wananchi kuelewa kuhusu masuala ya afya, huku akimtaka DMO kumrejeshea Sh15,000 mwananchi aliyetoa lalamiko hilo.
Kero nyingine iliyotolewa na wananchi ni ubovu wa barabara ya Isaka, ambapo Kihongosi amemtaka meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Joseph Mkwizu, kuitolea ufafanuzi kabla ya kutoa agizo kuwa ukarabati ufanyike mara moja kuanzia leo, Machi 5, 2026.
Changamoto nyingine iliyotolewa ni masuala ya ardhi ndani ya mipaka na hati, sambamba na tatizo la ukusanyaji wa taka katika makazi ya watu.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akisikiliza kero za wananchi Kahama.
Kihongosi amesisitiza kuwa mazingira machafu ni hatari kubwa, kwani huongeza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa kama kipindupindu, na akataka wahusika kushughulikia changamoto hiyo haraka ili kulinda afya ya wananchi.
Kero nyingine iliyotajwa ni ya upatikanaji wa mita za maji, wananchi wakidai wamelipia kwa miezi kadhaa lakini hadi sasa hawajapata huduma.
Kihongosi amemtaka mhusika wa Idara ya Maji kulitolea ufafanuzi, ambaye alikiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa mita kwa muda sasa, na kusema jitihada zinaendelea vizuri. Mzabuni aliyepewa kazi amewaahidi baada ya wiki mbili zitakuwa zimeletwa.
Kihongosi alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, na kumuuliza kama anafahamu kuhusu kero hiyo. Mtendaji huyo wa wizara aliomba aifanyie kazi, na Kihongosi kuahidi kulitolea majibu kabla hajaondoka Shinyanga.
Mbali na mkutano huo wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, mjini Kahama pia Kihongosi amekagua ujenzi wa bandari kavu na stendi mpya ya Mbulu.
Katika miundombinu hiyo, Kihongosi amesema inakwenda kuongeza uchumi wa Kahama, huku akisisitiza kutokuwepo kwa vishoka mara ujenzi wa stendi utakapokamilika na vibanda vya biashara kuanza kutolewa.