RAIS DKT. MWINYI AIHIMIZA BENKI YA KCB KUSHIRIKIANA NA SMZ KUWAWEZESHA VIJANA

…….

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumzia changamoto zinazowakabili vijana, ameisisitiza benki ya KCB Tanzania kupitia programu ya kurudisha fadhila kwa jamii kushirikiana na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kutafuta njia bora na endelevu zitakazowanufaisha vijana, hususan katika suala la uwezeshaji wa mikopo kwa vijana hili waweze kujiajiri.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 5 Machi 2026, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Tanzania, Ndg. Cosmas Kimario, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Peter Kallaghe, wakiongozana na watendaji wakuu wa taasisi hiyo waliofika Ikulu, Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameishauri Benki ya KCB Tanzania kufikiria uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata mikopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Ameeleza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa bandari, viwanja vya ndege na miundombinu ya barabara inahitaji fedha nyingi ili kukamilika kwa wakati, hivyo ameisisitiza KCB kulipa umuhimu suala hilo kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.

Aidha, ameihakikishia benki hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiwekea mpango madhubuti wa malipo ya fedha inazokopa kupitia akaunti maalum ya kulipa mikopo inayotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa KCB Tanzania, Ndg. Cosmas Kimario, amesema kuwepo kwa mazingira mazuri ya uwekezaji Zanzibar, ujenzi wa miundombinu na mkazo katika sekta za uchumi wa buluu na utalii kunakovutia wawekezaji wengi kuja nchini kumeisukuma benki hiyo kuongeza mtaji wake kwa ajili ya Zanzibar na wako tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.