……..
Tanzania inaendelea kujitangaza kimataifa katika maonesho ya utalii ya ITB Berlin 2026, ambapo Makumbusho ya Taifa laTanzania (NMT) inashiriki kikamilifu katika kampeni ya “Tourism Beyond Safaris.”
Katika maonesho hayo, NMT inatangaza vivutio vya utalii wa urithi wa historia na utamaduni kama vile Olduvai Gorge pamoja na magofu ya Kilwa Kisiwani na maeneo mengine ya kihistoria ya pwani ya Tanzania.
Sambamba na hilo, NMT kwa kushirikiana na Staatliche Museen zu Berlin na Humboldt Forum imeandaa maonesho maalum yaliyopewa jina la “Histories of Tanzania,” yanayoelezea historia ya Tanzania kabla ya ukoloni na wakati wa mawasiliano na Wajerumani kupitia vielelezo vya kiutamaduni.
Ujumbe wa NMT katika maonesho hayo uliwasilishwa na Mkuu wa Programu, Achilles Bufure, pamoja na Mkuu wa Masoko na Uhusiano, Pendo Gondwe, ambao wanatoa utaalamu kuhusu utalii wa urithi (Heritage Tourism), unaozidi kupata umaarufu miongoni mwa watalii wa Ulaya wanaotafuta uzoefu halisi wa kielimu, historia na utamaduni.
Kupitia ushiriki huo katika ITB Berlin, NMT inalenga kujenga ushirikiano wa kimkakati na wadau wa sekta ya utalii ili kuimarisha ujumbe wa Tanzania Beyond Safaris na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania

