Arusha. Macho na masikio ya wadau wa siasa, sheria na watetezi wa haki za binadamu kesho yataelekezwa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), inayotarajiwa kutoa hukumu katika kesi inayohusu madai ya ukiukwaji wa haki za kiraia na kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2020 nchini.
Kesi hiyo namba 046/2020 ilifunguliwa Novemba 20, 2020 na watu sita wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani na wapiga kura dhidi ya Serikali ya Tanzania, wakidai kuwa haki za msingi za kiraia na kisiasa zilikiukwa wakati wa mchakato wa uchaguzi huo.
Katika shauri hilo, waombaji waliongozwa na Seif Sharif Hamad (marehemu), aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Waombaji wengine ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, Ezekiah Wenje, aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Rorya, Omar Mussa Makame, aliyekuwa mgombea katika Jimbo la Kwahani, Dorah Wangwe, Enock Suguta pamoja na kundi la wapiga kura waliosajiliwa.
Kwa pamoja, waombaji waliwasilisha madai 12 katika mahakama hiyo. Miongoni mwa madai hayo ni kukamatwa kiholela kwa wagombea wa upinzani, kusimamishwa kwa kampeni zao pamoja na kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wa ubunge na udiwani.
Aidha, waombaji wanapinga uteuzi wa kada wa chama tawala kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakidai kuwa hatua hiyo ilidhoofisha uhuru na uaminifu wa taasisi hiyo muhimu katika kusimamia uchaguzi.
Madai mengine yanahusu kuwepo kwa vikwazo vya kisheria, vilivyodaiwa kuzuia pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya kutangazwa, vitendo vya vurugu dhidi ya wagombea wa upinzani na wafuasi wao, pamoja na madai ya rushwa ya kura na kujazwa kwa kura bandia kwenye masanduku ya kura.
Waombaji pia wanadai kulikuwepo na uhesabuji usio wa kawaida wa kura, kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari huru na kudhibitiwa kwa huduma za mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii katika kipindi cha uchaguzi.
Kwa mujibu wa waombaji, matukio hayo kwa pamoja yalidhoofisha uadilifu, uwazi na uaminifu wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Kutokana na madai hayo, waombaji wameiomba Mahakama itamke kuwa Tanzania ilikiuka wajibu wake chini ya mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa.
Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, pamoja na Itifaki ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Wanawake Barani Afrika, maarufu kama Itifaki ya Maputo.
Aidha, wanataka Mahakama ithibitishe kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki ya kushiriki katika uchaguzi, haki ya usawa, haki ya utu pamoja na haki ya ushiriki wa kiraia.
Waombaji pia wameiomba Mahakama kuamuru Serikali ya Tanzania kuwachukulia hatua wote waliohusika na madai ya ukiukwaji huo, pamoja na kuchukua hatua za kikatiba, kisheria na kiutawala ili kurekebisha kasoro zilizobainika katika mchakato wa uchaguzi.
Mbali na hilo, wameomba Serikali ilipe fidia kwa waombaji pamoja na kugharamia gharama zote za kesi hiyo.
Katika shauri hilo, waombaji wanawakilishwa na mawakili wa haki za binadamu akiwemo Chidi Odinkalu, Ibrahim Kane na Donald Deya.
Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, itawakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ally Possi akisaidiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Nkasori Sarakikya.