Siku tatu ngumu za Sowah Simba

NI takribani wiki moja imepita tangu taarifa za mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah ziripotiwe huku ikielezwa amesimamishwa kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.

Wakati muda huo ukipita huku kukiwa na ukimya kidogo, mapya yameibuka na kuelezwa uongozi wa klabu hiyo umempa siku tatu kuanzia jana hadi kesho Jumamosi ili kujibu mambo matano yanayohusu sakata la kusimamishwa kwake.

Wakati Simba ipo Dodoma ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wake, Dodoma Jiji iliyochezwa Februari 25, 2026 na kumalizika bila ya kufungana, Simba ilimrudisha Sowah jijini Dar kwa lengo la kukutana na uongozi wa klabu hiyo kufanya kikao ambacho wakati huo hakikufanyika baada ya kuahirishwa kwa sababu za kiuongozi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Simba, uongozi umemtaka Sowah kutoa majibu ndani ya siku tatu kuanzia jana wakati ishu ya kusimamishwa kwake na kutokuwepo kwenye kikosi ikiendelea palepale.

Katika mambo hayo matano anayopaswa kuyajibu ndani ya siku tatu, klabu inataka maelezo kuhusu kuchelewa kwenye mikutano kadhaa ya timu, kukataa kufanya mazoezi ya ziada, kuchelewa mazoezini, kusafiri kwenda Angola kucheza dhidi ya Petro Atletico akiwa amevaa jezi ya SL Benfica badala ya mavazi rasmi ya klabu. Mwisho ni kufanya faulo za makusudi zinazoweza kusababisha kadi nyekundu, ikiwemo kwenye mechi dhidi ya Azam FC na Espérance.

“Ndani ya siku hizi tatu baada ya kupokea maelezo yake ndiyo majibu yatatoka atapewa adhabu au nini kimeamuliwa, lakini haitapita muda huo,” kimesema chanzo hicho na kuongeza.

“Watu wanatakiwa kusubiri kuona uongozi utachukua uamuzi gani, lakini hii yote itaamuliwa kwa namna ambavyo majibu ya mchezaji yatakuwaje.”

Mtandao wa Ghana Web, umeripoti ishu ya Sowah kusimamishwa na Simba imekuwa ikizungumzwa maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Katika chapisho lake la Februari 27, 2026, mtandao huo umemnukuu mwandishi mmoja wa Ghana aliyefanyiwa mahojiano na kituo cha redio cha Angel FM nchini humo ambaye ameeleza namna alivyozungumza na Sowah juu ya sakata lake.

Mwandishi huyo aliyejikita zaidi katika kuandika habari za soka la Afrika kwa jumla, amenukuliwa akisema awali Sowah hakukubali kujibu tuhuma alizopewa hadi mwanasheria na wakala wake wawepo.

Desemba 17, 2025, Sowah na Allasane Kante, waliadhibiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya dhidi ya Azam FC, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 7, 2025.

Nyota hao waliotua Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu, wameshamaliza adhabu yao baada ya kukosekana mechi tano mfululizo zikiwamo nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Mashujaa, KMC na Tanzania Prisons. Nyingine ni ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Greenland. Tangu adhabu kumalizika, Simba imecheza mechi mbili dhidi ya Dodoma Jiji na Yanga ambazo zote matokeo ni 0-0, huku Kante akicheza zote wakati Sowah akisimamishwa.

Mshambuliaji huyo alitua Simba msimu huu akitokea Singida Black Stars nakiwango kizuri cha ufungaji alichokionyesha msimu uliopita akicheza kwa takribani miezi sita na kufunga mabao 13 katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara, kikawavutia Wana Msimbazi na kumsajili kwa matumaini ya kuongeza makali safu yao ya ushambuliaji.

Akiwa Simba, msimu huu timu hiyo ikiwa imecheza mechi 25 za mashindano tofauti (Ligi ya Mabingwa 10, Ligi Kuu Bara 11, Kombe la Mapinduzi 3 na Ngao ya Jamii 1), Sowah amecheza mechi 11 kwa dakika 477.

Mechi hizo ni Ligi Kuu Bara (4), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Kombe la Mapinduzi (1) ambapo Sowah amefanikiwa kufunga mabao matatu yote kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, JKT Tanzania na Mbeya City.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sowah alisema amepokea taarifa hiyo kwa heshima kubwa na kwa sasa anachosubiri ni uongozi wake ukutane na Simba.

“Ni kweli kuna hiyo barua lakini nimemwachia meneja wangu aifanyie kazi, siwezi kuongea zaidi.

“Natumaini wakati wowote kuanzia sasa viongozi watakutana na uamuzi utafanyika, ni hivyo tu,” alisema Sowah.

JKT Tanzania (dk 40 bao 1)

Mbeya City (dk 60, bao 1)