Dar es Salaam. Wakati gharama za mafuta zikitarajiwa kupanda kutokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati, Serikali imesema ujio wa magari ya umeme utaleta unafuu wa maisha kwa Watanzania.
Mzozo wa vita kati ya Marekani, Israel, na Iran umesababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani, ukizingatia kwamba Mashariki ya Kati inachangia asilimia 20 ya mafuta katika soko la dunia.
Kutokana na hilo, juzi Rais Samia Suluhu Hassan alisema: “Kama tunavyoona misukosuko iliyotokea wiki iliyopita na tunayoendelea nayo, tayari imeshapandisha bei ya mafuta kwa asilimia 13, sasa hatujui leo na siku zinazokuja. Tuombe watu wale wakae wazungumze.”
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, gharama ya kuendesha chombo cha umeme ni nafuu kuliko ile ya mafuta.
Ametolea mfano kwamba unaweza kutumia Sh100,000 kuendesha gari la mafuta, lakini kwenye umeme utatumia Sh15,000.
Mramba, ambaye anasimamia umeme na nishati jadidifu, amesema hayo leo Ijumaa, Machi 6, 2026, wakati wa uzinduzi wa magari ya umeme (EMVS) yanayosimamiwa na kuingizwa nchini na kampuni ya Zera.
“Wawekezaji hawa wamekuja wakati mwafaka sana. Kwa kuongeza idadi ya vyombo vinavyoendeshwa na umeme, pia wakati huu ambapo gharama za mafuta katika soko la dunia zinapanda,” amesema Mramba.
Kwa mujibu wa Mramba, mpaka sasa inakadiriwa kuwa magari 10,000, zikiwamo bajaji na pikipiki zinazotumia nishati ya umeme nchini, yana uwezo wa kutembea kilomita 300 kabla ya kuchaji tena.
“Tukienda na teknolojia hii, tutaleta unafuu mkubwa kwenye maisha ya watu, lakini pia tutahifadhi mazingira kwa sababu hayatoa moshi,” amesema Mramba.
Amesema wizara hiyo imejiandaa vizuri kuipokea teknolojia hiyo kuanzia upatikanaji wa umeme wa kutosha hadi ujenzi wa vituo vya kuchaji magari kila mahali ili kurahisisha huduma kwa Watanzania.
“Tumeshaanza mipango ya kuhakikisha mikoa mbalimbali ina vituo vya kuchaji magari. Ikitokea mtu ana safari kutoka Mwanza, anaweza akachaji Nzega, Dodoma, na Morogoro,” amesema Mramba.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zera, Emmanuel Kazimoto, amesema magari hayo yanatoka China na mpango mkakati ni kuanza kuyaingiza kwa mara ya kwanza, lakini baadaye kuyatengeneza hapa nchini.
“Tumeshapata hati ya uwekezaji na kiwanda chetu kitakuwa Kibaha (Pwani). Hatua ya kwanza ni uingizaji na usambazaji, hatua ya pili kuleta vipuri, kisha kuyaunda magari haya hapa nyumbani.”
“Kutakuwa na magari ya biashara na binafsi, yatakuja na yakiwa na kilomita sifuri,” amesema Kazimoto.
Katika hatua nyingine, Kazimoto ameiomba Serikali kuwapunguzia kodi kwenye vipuri vya kuchaji magari hayo, ili kuwezesha Watanzania wengi kuvimudu.