Ufugaji watajwa chanzo cha magugu maji Ziwa Victoria

Dodoma. Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria imeeleza kuwa shughuli za kibinadamu, hususan ufugaji, ndicho chanzo kikuu cha magugu maji katika Ziwa Victoria.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Machi 6, 2026, na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji wa Bonde la Ziwa Victoria, Dk Renatus Shinhu, wakati akielezea shughuli zinazofanyika katika bonde hilo.

Dk Shinhu amesema bila jamii kusimamia mkakati wa kujali na kuona thamani ya maji kama ilivyo katika mataifa mengine, hali itazidi kuwa mbaya.

Amesema bodi imeweka mkakati madhubuti wa kumaliza tatizo la magugu maji, lakini wanakutana na changamoto ya uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa maji kwa faida yao.

“Watu wanatakiwa waone umuhimu wa utunzaji wa maji. Ziko nchi za wenzetu kama Misri ambapo utamaduni wao jambo la kwanza ni utunzaji wa maji. Sasa nasi tukiamua kusimamia hapo, lazima maziwa na mito yetu itakuwa safi,” amesema Dk Shinhu.

Mkurugenzi ameeleza kuwa moja ya mikakati ya kulinda vyanzo hivyo ni kujenga vizingiti na vigingi vya kulinda vyanzo vya maji, ambapo hadi sasa wamejenga mipaka kwenye vyanzo 25.

Akizungumzia matumizi ya maji ya Ziwa Victoria, amesema hadi sasa wameshatoa vibali 1,396 kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mazingira, na shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Dk Shinhu, Tanzania inayomiliki asilimia 43 ya ziwa lote la Victoria, imeweka mkakati wa mfano katika kutunza mazingira ya vyanzo vya maji na ulinzi wa ziwa hilo, ambalo ni chanzo cha Mto Nile.

Kuhusu matumizi ya maji, amesema hadi sasa mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, na Geita, miji yao inategemea zaidi maji ya Ziwa Victoria, lakini Bomba la Maji limeshafika eneo la Shelui mkoani Singida, ambao nao wameanza kuyatumia.