Maofisa elimu wakumbushwa nidhamu, itifaki kazini

Dar es Salaam. Wakati jitihada za kuboresha sekta ya elimu nchini zikiendelea kuchukua nafasi kubwa katika mijadala ya kitaifa, viongozi wa elimu wametakiwa kuzingatia nidhamu, itifaki na tabia njema ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo.

Wito huo umetolewa jijini Arusha katika Mkutano Mkuu wa 12 wa Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara (REDEOA), unaoendelea kwa siku saba tangu ulipofunguliwa rasmi Machi 2, 2026, na Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe.

Mkutano huo umewakutanisha maofisa elimu kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali pamoja na wadau wa sekta ya elimu, kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayolenga kuboresha utendaji na kuongeza matokeo chanya katika sekta hiyo.

Akitoa mada kuhusu Itifaki na Tabia Njema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk Maulid Maulid, amesema viongozi wanapaswa kuishi kwa kuzingatia misingi ya nidhamu, utii wa sheria, na kufuata taratibu pamoja na kanuni zinazosimamia utendaji wa kazi serikalini.

Amesema kuzingatia itifaki na tabia njema ni msingi muhimu unaojenga mahusiano mazuri kati ya viongozi na wadau wa sekta ya elimu, jambo linalochangia kufanikisha utekelezaji wa malengo ya sera za elimu.

“Taswira njema ya utumishi wa umma hujengwa kupitia nidhamu na tabia njema za viongozi. Hivyo, ni muhimu kwa wasimamizi wa sekta ya elimu kuwa mfano bora kwa wengine,” amesema Dk Maulid.

Ameongeza kuwa kuimarishwa kwa itifaki kutasaidia kuongeza weledi, uwajibikaji, na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ndani ya sekta ya elimu.

Dk Maulid amewahimiza viongozi wa elimu kuwa mabalozi wa maadili mema na utendaji unaozingatia taratibu, ili taasisi wanazoziongoza ziweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu wamesema mjadala wa itifaki na tabia njema kwa viongozi wa elimu ni muhimu hasa katika kipindi ambacho sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji na uwajibikaji.

Mchambuzi wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Leonard Maganga, amesema viongozi wa elimu wanapokuwa na nidhamu na kuzingatia itifaki, huongeza uaminifu kwa walimu, wanafunzi, na jamii kwa ujumla.

“Maofisa elimu ndiyo daraja kati ya sera za serikali na utekelezaji wake shuleni. Kama hawataonesha maadili ya uongozi, utekelezaji wa sera hizo unaweza kukosa ufanisi,” amesema.

Kwa upande wake, mtafiti wa sera za elimu, Mary Minja, amesema mara nyingi changamoto katika sekta ya elimu hazitokani tu na uhaba wa rasilimali, bali pia na namna viongozi wanavyosimamia mifumo ya kazi.

Amesema viongozi wanaozingatia maadili na itifaki hujenga mazingira ya uwazi na uwajibikaji, jambo linalosaidia kupunguza migogoro na kuongeza ufanisi katika taasisi za elimu.