Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, imekuja na mikakati maalumu ya kufanya tathmini na kutenga bajeti ya Sh2.5 bilioni kukamilisha miradi viporo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kauli hiyo imekuja leo Machi 6, 2026, baada ya wananchi wa Kata ya Kongoro Mswisi, wilayani humo, kuiangukia halmashauri kuomba kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali, ikiwepo zahanati yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 4,873, ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2018.
Ombi hilo limetolewa kwenye mkutano wa hadhara ulioratibiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, wa kusikiliza kero za wananchi, ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Serikali.
Mbali na kusikiliza kero za wananchi, Mweli alifanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika sekta ya afya na elimu, na kueleza kuwa halmashauri imechangia Sh45 milioni, kati ya hizo Sh40 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kongoro na Sh5 milioni kwa ukarabati wa chumba cha darasa katika Shule ya Msingi Mkola.
“Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, tumejipanga kutenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha miradi yote viporo, lakini hatuwezi kuendelea kujenga mipya. Lengo ni kuona iliyopo inakuwa na tija kwa kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mweli.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyo zunguka Kata ya Kongoro Mswisi kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi. Picha na Hawa Mathias
Amesisitiza kuwa Serikali imewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wananchi wanafikiwa na kusikilizwa kero zao kwa kutokaa maofisini.
“Ndugu zangu wana Mbarali, tangu niteuliwe na Rais kushika kipande hiki, niwahakikishie ninafikika na hakuna kizuizi chochote. Ukiwa na shida, njoo ofisini kwangu tutazungumza, na endapo kukiwa na vikwazo, toeni taarifa, nipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi,” amesema.
Mweli amesema lengo la Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi, jambo ambalo atahakikisha jamii inafikiwa na miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kubwa kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mweli amehamasisha wananchi kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo yenye riba ya asilimia 10, na kubainisha kuwa kwa mwaka huu zaidi ya Sh738 milioni zimetolewa, huku Sh600 milioni zikisalia.
“Mbali na kutoa kiasi hicho cha mikopo, bado tuna kiasi cha Sh600 milioni kinasubiri wakopaji. Hivyo, wananchi changamkieni fursa, jiungeni kwenye vikundi kuja na wazo ili mnufaike kwa kuanzisha miradi, hususan katika sekta ya kilimo,” amesema.
Amesema Serikali, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, wanaendelea kujenga skimu 100 kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati, likiwepo zao la mpunga.
“Halmashauri inategemea mapato ya asilimia 80 kutoka sekta ya kilimo, ikiwemo zao la mpunga, jambo ambalo linatoa msukumo wa kuboresha miundombinu ya sekta hiyo,” amesema.
Diwani wa Kongoro Mswisi, Leonard Mwampyate, ameishukuru halmashauri kwa kuunga mkono juhudi za wananchi, kuchangia Sh40 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, jambo litakaloondoa adha ya kutembea umbali mrefu.
“Mkurugenzi, nikushukuru kwa kufika kujionea hali halisi ya miradi ya maendeleo, lakini pia kutoa kauli ya matumaini kwa wananchi kwa kuja na mpango mkakati wa kukamilisha miradi yote viporo sambamba na kupeleka walimu katika shule zetu shikizi,” amesema.
Mkazi wa Kijiji cha Azimio, kilichopo katika Kata ya Kongoro, Hamis Mbasha, ameomba Serikali kupeleka walimu kwenye shule shikizi, jambo ambalo halmashauri imeahidi kulifanyia kazi ndani ya wiki mbili.
Mkazi wa kata hiyo, Jesca Amos, amesema kutokana na kuchelewa kukamilika kwa mradi huo, wamekuwa wakipata adha kubwa ya kusafirisha umbali mrefu kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Chimala.