Dar es Salaam. Wakati zaidi ya Watanzania 800,000 wakiwa wamewekeza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), imeelezwa kuwa wanawake ni asilimia 35 ya wawekezaji katika soko hilo mpaka sasa.
Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Machi 6, 2026 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, wakati wa hafla ya upigaji kengele maalumu inayolenga kuikumbusha jamii umuhimu wa usawa wa kijinsia. Hafla hiyo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 9 ya kila mwaka.
Nalitolela amesema licha ya idadi ya wawekezaji kufikia zaidi ya 800,000, akaunti zinazomilikiwa na wanawake ni 281,000, hali inayodhihirisha kuwa bado idadi yao ni ndogo ikilinganishwa na wanaume.
Amefafanua kuwa hali hiyo ina mizizi ya kihistoria, kwa sababu kwa muda mrefu wanawake wamekuwa nyuma katika shughuli za kiuchumi, si Tanzania pekee, bali pia katika nchi nyingi duniani.
“Tatizo hili la ushiriki mdogo wa wanawake katika uwekezaji lina asili ya kihistoria. Kwa muda mrefu katika familia na jamii, baba ndiye aliyekuwa msimamizi wa shughuli nyingi za kiuchumi. Hata tulipoingia katika mfumo wa uchumi wa kisasa wa masoko, bado baadhi ya mitazamo hiyo imeendelea kuwepo,” amesema Nalitolela.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wanaume wengi ndio waliokuwa wa kwanza kufungua akaunti za uwekezaji wakati masoko ya mitaji yalipoanza kuimarika.
Hata hivyo, Nalitolela amesema DSE imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uwekezaji wa soko la hisa, ikiwamo kutoa elimu na kuhamasisha wanawake, wasichana na wadada kufungua akaunti za uwekezaji pamoja na kutumia soko hilo kama chanzo cha kupata mitaji ya kukuza biashara zao.
Amesema awali wawekezaji walilazimika kufungua akaunti kupitia mawakala, jambo lililowawia vigumu baadhi ya wanawake. Hata hivyo, kwa sasa huduma hiyo imeboreshwa kwa kutumia teknolojia ya kidijitali inayomwezesha mtu kufungua akaunti kwa urahisi kupitia simu au akiwa nyumbani.
“Kwa sasa tumerahisisha huduma hizi kwa kuziweka kidijitali, hivyo mwanamke anaweza kufungua akaunti hata akiwa nyumbani. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika uwekezaji,” amesema.
Aidha, amesema DSE itaendelea kutoa elimu ya uwekezaji kwa wanawake kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwamo mikutano ya vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba), ili kuwahamasisha kushiriki katika uwekezaji huo unaoweza kusaidia kukuza uchumi wao binafsi pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji (CMSA), Dk Martin Wilbert Kolikoli, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema usawa wa kijinsia umeainishwa kisheria na hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha unazingatiwa katika mazingira ya kazi na jamii kwa ujumla.
Amesema taasisi yake ina jukumu la kuchochea usawa huo katika sekta ya masoko ya mitaji na tayari imeanza kutekeleza mifumo na sera zinazolenga kuhakikisha kila mtu anapata fursa sawa.
Akizungumzia ushiriki mdogo wa wanawake katika uwekezaji wa soko la hisa, Dk Kolikoli amesema kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki katika uwekezaji huo, kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza soko la mitaji pamoja na kuongeza kampuni zenye ushiriki wa wanawake.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Global Compact Network Tanzania, Marsha Macatta-Yambi, amesema lengo la kuandaa hafla hiyo ni kuzikutanisha kampuni mbalimbali ili kujadili na kuimarisha utekelezaji wa usawa wa kijinsia katika shughuli zao za kila siku.
Macatta-Yambi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati iliyoratibu hafla hiyo, amesema pamoja na mambo mengine kampuni zimehimizwa kujitathmini ili kubaini kama zinaweka usawa wa kijinsia katika ajira na uendeshaji wa shughuli zao.
“Katika jukwaa hili tunazipa kampuni mbinu mbalimbali, ikiwamo namna ya kutumia takwimu, kupanga mikakati ya usawa wa kijinsia na kufanya tathmini ya ndani ili kubaini maeneo wanayofanya vizuri na yale yanayohitaji maboresho,” amesema.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa ukosefu wa usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi unaweza kuathiri ufanisi wa utendaji, hivyo ni muhimu taasisi na kampuni kuhakikisha zinajenga mazingira jumuishi yanayotoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume.