RC Mara ashusha zigo la elimu ya udumavu kwa wahudumu wa afya

Musoma. Wakurugenzi wa halmashauri tisa za wilaya mkoani Mara, wametakiwa kutenga bajeti ya kuwezesha angalau wahudumu wawili wa afya ngazi ya jamii katika kila kijiji na mtaa, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na lishe bora kwa wananchi.

Pia, wametakiwa kuhakikisha maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe Vijijini yanafanyika katika vijiji vyote, badala ya kufanyika katika halmashauri moja pekee kama ilivyo sasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

Maagizo hayo yametolewa leo Ijumaa, Machi 6, 2026 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi wakati akifungua kikao cha tathmini ya hali ya lishe mkoani humo.

Kanali Mtambi amesema kiwango cha udumavu mkoani Mara kwa sasa ni asilimia 23.4, licha ya kuwa chini ya wastani wa taifa wa asilimia 30, bado ni kiwango kinachohitaji juhudi zaidi kupunguzwa.

“Ingawa tuko chini ya kiwango cha taifa ambacho ni asilimia 30, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kupunguza kiwango hiki. Hili linawezekana endapo tutatekeleza kikamilifu afua zote za lishe,” amesema.

Amesema uwepo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kila kijiji na mtaa utasaidia kufikisha ujumbe sahihi wa lishe bora kwa walengwa, jambo litakalosaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya lishe na afya.

Aidha, amesema mapambano dhidi ya udumavu ni ajenda ya kimataifa kwani nchi nyingi duniani zinaweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo, ambalo huchangia kuendelea kwa mnyororo wa umasikini katika jamii na taifa kwa ujumla.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe Vijijini, amesema yakifanyika katika ngazi za vijiji yataongeza uelewa kwa wananchi, hususan kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto wadogo na mama wajawazito.

Kanali Mtambi pia ameagiza shule zote za umma kuwa na mashamba darasa yatakayosimamiwa na maofisa ugani katika maeneo husika, ili kusaidia kuongeza upatikanaji wa chakula shuleni sambamba na kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu kilimo na lishe bora.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Mara, Benson Sanga amesema uwepo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya udumavu pamoja na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Amesema ili wahudumu hao waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, halmashauri zinapaswa kutenga bajeti ya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Sisi tumeandaa muongozo kwa ajili ya wahudumu hawa ili waweze kufika hadi ngazi ya familia kutoa elimu na hamasa. Kinachohitajika sasa ni kuwawezesha ili wawafikie walengwa kwa ufanisi,” amesema.

Sanga amesisitiza kuwa lishe bora kwa watoto ni jambo la msingi kwa maendeleo ya taifa, kwani uwekezaji katika lishe ya watoto unachangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk Osmund Dyegura amesema mapambano dhidi ya udumavu yanapaswa kuwahusisha pia watoto wenye umri chini ya miaka minne, ambao takwimu zinaonyesha ndio wanaoathirika zaidi.

“Kwasasa nguvu nyingi zimeelekezwa kwa watoto waliopo shuleni, lakini tunawasahau wale waliopo nyumbani. Ni muhimu juhudi zielekezwe pia kwa kundi hilo ili tatizo hili lipate ufumbuzi wa moja kwa moja,” amesema.